TAARIFA YA POLISI MKOA WA DODOMA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi David Misime(pichani)
ameeleza kuwa kutokana na tukio la kihistoria ambalo litafanyika tarehe
08.10.2014 ambapo Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mh. Rais wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watakabidhiwa Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma
hususani Dodoma Mjini.
Ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali na
kuzifanyia kazi umeimarishwa zaidi, doria za miguu, magari, pikipiki na mbwa na
farasi nazo zimeimarishwa. Pia vyombo vyote vya dola tumeimarisha zaidi
ushirikiano hasa kubadilishana taarifa mbalimbali na wote mitaani kufuatilia
tukio hili muhimu kwa kutumia mbinu zote walizo nazo.
Niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa
Dodoma na wageni wote kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa tunachowaomba ni
ushirikiano wao pale watakapomtilia mashaka mtu yeyote au jambo lolote wajulishe Polisi haraka nao watalifanyia
kazi. Pia wenye nyumba za kulala wageni waimarishe ulinzi kwenye maeneo yao ya
biashara na kuwapa maelekezo sahihi wafanyakazi wao na wakitilia shaka mgeni
yeyote watoe taarifa polisi.
Pia wananchi wote pamoja na wageni wote
watii sheria bila shuruti na yeyote anayepanga kukiuka sheria ili kuvunja amani
na utulivu atashurutishwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za nchi na kwa
mamlaka waliyopewa Jeshi la Polisi.
Imetolewa na Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma.
0 comments:
Post a Comment