Majadiliano juu ya ombi la Sudani
Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yameahirishwa hadi Oktoba
mwaka huu, Mkutano wa wakuu wa nchi EAC ulisema Jumatano.
Mwenyekiti wa
Mkutano huo,Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema mjini hapa kwamba
kucheleweshwa huko kutatoa nafasi kwa Sudani Kusini kufanya maandalizi ya
kitaifa na mashauriano.
‘’Hata hivyo EAC
imeshafanya maandalizi ya utaratibu na mpango wa majadiliano na Jamhuri ya
Sudani Kusini juu ya nchi hiyo kuingizwa katika jumuiya,’’ Kenyatta alisema
wakati wa kikao Maalumu cha 12 cha wakuu wa EAC.
Alisema kuwa
mgogoro uliozuka Sudani Kusini mwaka jana, bado unaendelea katika baadhi ya
maeneo nchini humo.
‘’Hayo yanatokea
licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini na pande
zinazohusika katika mgogoro huo mapema mwaka huu,’’ alisema Kenyatta.
Kiongozi huyo wa
Kenya alisema EAC inatoa wito madhubuti kwa pande zinazopigana kuheshimu hadidu
za rejea za makubaliano ya amani yaliyofikiwa,linaripoti Shirika Huru la Habari
la Afrika Mashariki (EANA).
Wakati huohuo
Baraza la Mawaziri la EAC juzi lilisema kwamba asilimia 57.9 ya maamuzi na
maelekezo ya wakuu wa nchi wanachama yemetekelezwa mpaka sasa.
Mwenyekiti wa
Baraza la Mawaziri wa EAC, Phyllis Kandie alikiambia kikao Maalumu cha 12 cha
Wakuu wa Nchi za EAC kwamba jumla ya maamuzi na maelekezo 121 yametekelezwa
wakati wa vikao vya kawaida na vikao maalum vya EAC tangu mwaka 2001.
‘’Hata hivyo,
asilimia 42 ya maamuzi yakiwakilisha asilimia 34.7 yameshughulikiwa kinusunusu
wakati mengine 9 au asilimia 7.4 yakiwa bado hayajaguswa kabisa,’’ alisema
Kandie.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa EAC, Rais Kenyatta alitoa wito
kwa nchi wanachama pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kutekeleza haraka mambo
ambayo bado hayajakamilishwa.
0 comments:
Post a Comment