Nafasi Ya Matangazo

May 12, 2014



Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Dar Brew maarufu zaidi kama Chibuku, imezindua rasmi bia mpya ya asili ijulikanayo kama ‘Chibuku Super’, ambayo imewekwa katika chupa maalumu ambayo mteja anaweza kuondoka nayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Dar Brew, Kirowi Suma, alisema wanaingiza bidhaa hiyo mpya sokoni iliyo na ubora wa hali ya juu, huku ikiwa na uwezo wa kukaa sokoni kwa muda mrefu zaidi.

Suma alisema, kinywaji hicho kitauzwa kwa sh. 1,200 na ikiwa na ujazo wa lita moja, huku kikiwa hakina kemikali yoyote, kwani kimetengenezwa kwa kimea halisi, huku mtumiaji akiweza kutumia bila kukumbwa na mzio wowote ule.

“Leo (jana) ni siku ya furaha kubwa sana kwetu Dar Brew na kwa watumiaji wote wa bia, kwani tumeweza kinywaji kipya cha Chibuku Super ambayo inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika soko la bia hapa nchini.

“Bia hii imetengenezwa kwa utaalam wa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa, hivyo kuwahakikishia wanywaji ubora wa hali ya juu,” alisema Suma.

Alisema, bia hiyo inatengenezwa kwa kutumia malighafi za Tanzania, ikiwemo nafaka ya mtama ulio bora toka kwenye ardhi yetu, huku akitaka Watanzania kujivunia kilicho chetu na kukumbuka asili yetu.

“Chibuku Super ina kilevi cha asilimia 4, kinachokufanya uweze kuitumia kwa muda mrefu ukiwa na marafiki, lakini pia inakupa lishe nzuri kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika nafaka zinazotumika kutengeneza bia hii.

“Kwa sasa bia hii itaanza kupatikana katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma, kisha itaenea nchi nzima.”

Akizungumzia juu ya usambazaji, Meneja Mauzo wa Dar Brew, Saidi Mremi, alisema Chibuku Super itaanza kupatikana leo katika baa zote, maduka makubwa na sehemu nyinginezo zinazouza vileo.

“Tuna imani kubwa wapenzi wa bia wataipokea bia hii mpya kwa shangwe na furaha kubwa na pia watatumia bia hii kuonesha kuwa wanajali asili yao.”

Uzinduzi huo uliojawa na burudani zisizo kifani, ilihudhuriwa na wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo Ubungo, wauzaji wa jumla na rejareja na wageni wengi waalikwa.

wan
Posted by MROKI On Monday, May 12, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo