Mratibu
wa uhurumarathon nchini Bwana Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar Es Salaam juu maandalizi ya mbio hizo mwaka huu na umuhimu wa
kulinda na kuenzi amani ya taifa la Tanzania ambapo mbio hizo mwaka huu
zitafanyika jijini Dar Es Salaam na zitazinduliwa Butiama mkoani Mara.
******
Na Mwandishi
Wetu
MBIO za Uhuru (Uhuru Marathon) zinatarajiwa
kuzinduliwa rasmi katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, Agosti mwaka huu, huku
lengo kubwa likiwa ni kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Mratibu wa Uhuru Marathon, innocent Melleck alisema, wameamua
kuzindulia Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye
katika uhai wake alipigania mno mambo hayo.
“Tukumbuke Mwalimu Nyerere alipigania mno amani,
umoja na mshikamano miongoni mwetu, pia ndiye muasisi wa Taifa hili, hivyo
tuliona bora tukazindulie Butiama ili kumuenzi.”
Alisema, mara baada ya uzinduzi huo wanatarajia
kuzunguka nchi nzima kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuzitambulisha mbio hizo na
kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
Melleck alisema, kiini cha kuanza kampeni ya
kuzindua mbio hizo mapema imekuja, kwani zenyewe zimebeba ujumbe wa amani,
umoja na mshikamano, hivyo ni vyema kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kutunza
na kuenzi mambo hayo.
“Amani ya nchi yetu katika siku za hivi karibuni
inaonekana kwenda vibaya hasa kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kufanya
siasa kwa visasi badala ya kujenga hoja kukabiliana na changamoto za kisiasa,
hivyo ni jukumu letu kuilinda,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT), Selemani Nyambui alisema, kuanza maandalizi mapema kwa mbio hizo ni
faraja kwao na watahakikisha wanakabiliana na changamoto zote ili ziweze
kufana.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 8, mwaka
huu na kwa mara ya kwanza zilifanyika mwishoni mwa mwaka jana na kushirikisha
wanariadha kutoka nchi mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment