WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Jumuiya ya Wazazi
nchini ni miongoni mwa jumuiya inayoongoza na kusimamia masuala yote yanayohusu
elimu, malezi bora kwa vijana wa taifa letu hivyo lazima iangalie jinsi ya
kuweza kujipambanua katika utekelezaji wa Umoja wa Jumuiya yao.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumamosi, Februari
22, 2014), wakati akifungua rasmi semina ya siku tatu ya viongozi na watendaji
wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya Tanzania
inayofanyika kwenye Ukumbi wa NEC, Mkoani Dodoma.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu Pinda
aliwaeleza wana jumuiya hao kuangalia malengo wanayojipangia aidha yawe
ya muda mfupi au mrefu ili kuyatekeleza kwa kuzingatia yale mambo ya msingi na
yenye kipao mbele kwa wananchi.
“Changamoto kubwa iliyopo mbele yenu kama viongozi na
watendaji wakuu wa Jumuiya hii ni namna ya kutimiza malengo mliyojiwekea“.
Alisema, dhana ya Jumuiya ya Umoja wa Wazazi nchini ni
kuongeza na kuboresha masuala yote yanayohusu Sekta ya elimu hapa nchini:
‘‘Tumieni semina hii kujipima kwamba mmefikia wapi katika utelelezaji wa
malengo yenu kwa kuangalia mapungufu na maboresho katika jumuiya yenu‘‘.
Jumuiya ya Wazazi ndio magwiji mnaoongoza kwa kuwa na
shule nyingi hapa nchini, hivyo jumuiya yenu ijipange na kusimamia vema shule hizo
ili kuwa vinara katika kuboresha masuala ya elimu hapa nchini. Akitoa mfano,
alisema: “Kwanini shule za binafsi zinakuwa zinaongoza kuliko shule zilizopo
ndani ya Jumuiya yenu, walau katika kumi bora iwepo shule moja kutoka Jumuiya
ya Umoja wa Wazazi alisema Waziri Mkuu”.
Kutokana na kauli hiyo, Waziri Mkuu aliiambia Jumuiya
hiyo kutumia dhana ya elimu kama ngao yao katika kuleta maendeleo katika Sekta
hiyo kwani Ilani ya chama cha Mapinduzi imetamka wazi kuongeza kasi ya upanuzi
wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari lengo ambalo ni moja ya jukumu kuu la
msingi la Jumuiya ya Umoja wa Wazazi.
Aliendelea kusema kuwa Jumuiya ya Wazazi inajukumu la
kusimamia masuala yote yanayohusu maadili, jukumu ambalo halina tofauti sana na
jukumu la madhehebu ya dini kuzungumza bayana masuala ya malezi ya watoto na
vijana ambayo yamekuwa yakiporomoka kila kukicha, hivyo Waziri Mkuu alisema, jumuiya
hii itumia jukumu na nafasi waliyopewa kuhakikisha watoto wote walio ndani na
nje ya jumuiya wanafundishwa maadili.
Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa, Jumuiya ya Umoja wa
Wazazi ina majengo, viwanja na ardhi inayofaa kwa kilimo na shughuli za
kiuchumi, tumieni fursa hizi kwa kujenga vyuo, kuanzisha miradi ya maendeleo
ambayo itawasaidia katika kuongeza kipato katika jumuiya yenu.‘‘Mnachotakiwa ni
kupanga bajeti zenu vizuri na kusimaia utekelezaji pamoja kusimamia vizuri
miradi na fursa zinazojitokea“
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu aliiomba Jumuiya ya Wazazi
kujitokeza kuzungumzia masuala ya Dawa za Kulevya kwa kusema kuwa, wako vijana
ambao wametumbukia katika dimbwi la Dawa za Kulevya ambaa pia wanahatarisha
maisha yao kwa kupata UKIMWI: “Ni matumaini yangu kwamba Jumuiya ya Umoja wa Wazazi
itakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii, kutoa ushauri kwa vijana kuhusu
athari za dawa za kulevya, UKIMWI na
hata mkiweza kuanzisha vituo vya ushauri”, alisisitiza Waziri Mkuu.
“Ili kuweza kuwa na Jumuiya ya Wazazi imara ni dhahiri
kuwa wanajumuiya wasimamie kanuni na maadili yanayoongoza jumuiya yao kwa
kuwaasa kuacha kujiingaza katika makundi yasiyokuwa na msingi hasa kwa
kutanguliza maslahi ya fedha katika kupata nafasi za uongozi katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi mkuu ambao huleta migawanyiko kati ya Viongozi na
wanachama na wapiga kura”. Mzingatie masuala yanayohusu kujenga na kukuza
utekelezaji wa jumuiya yenu ambayo itawasaidia kujenga jumuiya imara na kujenga
chama imara kitakacho leta viongozi imara”alisisitiza Waziri Mkuu.
Mapema,
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Taifa, Bw. Majura Bulembo, alisema
lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo na kuwaongeza ufanisi Jumuiya ya
Wazazi katika utekelezaji kazi zao na
kuwasisitiza kuhudhuria semina hiyo ipasavyo ili kuweza kukumbusha mapungufu na
changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
0 comments:
Post a Comment