Nafasi Ya Matangazo

December 13, 2013

 Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya mwaka 2013 ambayo hutolewa kila mwaka na  Shirika la Afya Duniani,  Balozi aliwaeleza wageni waalikwa katika hafla hiyo kwamba ushiriki wa viongozi wa afrika kupitia mtandao wao wa  ALMA umechangia sana katika kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria
Dkt. Robert Newman kutoka WHO yeye amesema,  inasikitisha  pale inapobidi mtoto apoteze maisha kwa sababu tu  ameshindwa kupatiwa chandarua  ambayo  thamani yake ni dola tano. amewataka  viongozi na washirika mbalimbali kutobweteka na mafanikio katika kuudhibiti ugonjwa huo   mafanikio nayohusu kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa malaria na vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Bw, Ray Chambers ambaye ni Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema inatia moyo sana kuona vitanda katika wadi za watoto vikiwa vitupu mahali ambapo watoto walikuwa wakilala wawili katika kitanda kimoja kutokana na  kusumbuliwa na malaria.
 Dkt. Fatoumata Traore ambaye ni  Mkurugenzi mtendaji wa Roll Back Maralia akizungumza wakati wa halfa hiyo.
Katibu Mtendaji wa ALMA  Bi. Joy Phumapi naye  akizungumza machache 
*********
Na  Mwandishi Maalum
Utashi wa kisiasa  unaoonyeshwa na  marais wa Afrika  katika kudhibiti ugonjwa wa malaria, pamoja na ushiriki wa wadau mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Ban Ki  Moon  umeanza kuzaa  matunda kufuatia taarifa za kutia matumaini  zinazoonyesha  kupungua kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya   mwaka 2013 ya   Shirika la  Afya la Dunia ( WHO ) kuhusu mwelekeo wa ugonjwa wa  malaria katika kipindi  hicho , Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi amesema hapana shaka kwamba  mwamko ulioonyeshwa na Marais wa Afrika kupitia muungano wao dhidi ya  Malaria ( ALMA) umechangia   kwa kiasi kikubwa.

Jana  Alhamis   Bw. Ray Chambers ambaye ni mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Malaria kwa pamoja na  Dkt. Robert Newman ambaye ni  Mkurugenzi wa mradi wa Malaria (WHO), Bi.  Fatoumata Traore Mkurugenzi Mtendaji wa Roll Back Malaria na Bi.  Joy Phumapi ambaye ni Katibu Mtendaji wa ALMA walizindua  ripoti hiyo mbele ya  Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi za Afrika na wadau wadau wengine.

Akiwakaribisha wageni waalikwa kwa   niaba ya Balozi wa Msumbiji katika hafla hiyo iliyoandaliwa na ALMA, Balozi Manongi alisema     ripoti za kila mwaka za WHO zimekuwa zikionyesha mwelekeo mzuri katika  kuushughulikia ugonjwa huo ambao  unaadhiri kwa kiasi kikubwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano. Na kusisitiza kwamba Afrika inatakiwa kuzitumia ripoti hizo kuongeza kasi katika kuikabili Malaria.

“Ripoti hizi zinaonyesha kwamba tukishirikiana tunaweza kabisa kuidhibiti malaria, viongozi wetu wameonyesha mfano kwa kuanzisha muungano wao dhidi  ya malaria, ni wajibu wetu kuendelea kukusanya nguvu na kujituma Zaidi ili tusirudi nyuma” akasisitiza Balozi Manongi.

Ripoti ya malaria kwa mwaka huu, ambayo ni mkusanyiko wa taarifa kutoka nchi 102 zikiwamo  10 ambazo zimeathirika sana na ugonjwa wa malaria  na taarifa kutoka  vyanzo vingine,   inatoa tathmini  ambayo pamoja na mambo mengi  kwamba onyesha   ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na wafadhili  umewezesha  katika kipindi cha mwaka 2000-2012 kuokoa maisha ya   watu 3.3  milioni ambayo yangepotea kutoka na ugonjwa huo.

Taarifa hiyo inaeleza  Zaidi   kwamba ugonjwa wa  malaria umepungua kwa asilimia 45  duniani kote na kwa asilimia 49 katika nchi za Afrika   zinazohudumiwa na WHO.

Akizungumza katika uzinduzi huo Dkt. Robert  Newman kutoka WHO amewaeleza   Mabalozi kwamba ripoti  inahabari njema kuwa ugonjwa wa malaria umepungua kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi hicho cha kati ya 2000-2012

“ kuna punguzo la asilimia 54 la vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano vitokanavyo na malaria katika nchi za afrika  hususani zile ambazo zimeathirika Zaidi.  Takwimu hizi na nyingine zilizomo katika  ripoti hii zinathihirisha wazi kwamba  tukishirikiana tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika kuikabili Malaria” akasema Dkt Newman

Akaongeza kwamba  licha   utashi wa kisiasa ulioonyeshwa na viongozi  mbalimbali kumekuwapo na mwitikio unaoridhisha wa uchangiaji wa raslimali fedha katika eneo hilo. Ambapo katika kipindi hicho jumla ya dola za kimarekani bilioni mbili  zilitolewa na  wafadhili na  dola milioni mia tano zilitolewa na  nchi ambazo zimeathirika Zaidi. 

Hata hivyo akasema ingawa  mwamko wa kuchangia umekuwa mkubwa   bado lengo halijafikiwa  la kiasi cha dola   za kimarekani 5.1 na kuonya kwamba  bado michango inahitaji na wala mafanikio hayo yaliyopatikana yasijewafanya wadau wakabweteka kuchangia au kuhamishia fedha  kwenye masuala mengine.

“ hatupashwi kubweteka au kuridhika na mafanikio haya, haipendezi mtoto au mtu kufariki kwa sababu tu ya kushindwa kuwa na uwezo   wa kununua chandarua ambayo thamani yake ni sawa na dola tano ya kimarekani. Na weza kusema  mafaniko haya ni sawa na nusu glasi. Hebu  pata picha kama wewe ungekuwa ni mtoto unayeishi katika maeneo ambayo yameathirika vibaya na malaria halafu hakuna hata  dawa za kukutibu, bila  shaka matarajio yako ni kuona glasi imejaa na si nusu glasi au glasi iliyotupu” akasisitiza Muwakilishi huyo wa WHO.

Naye Mjumbe  Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu  Malaria na ambaye  amekuwa mstari wa mbele katika kuchagiza na kutafuta   raslimali zikiwamo fedha kwaajili ya miradi ya malaria, Bw. Ray Chambers alikuwa na haya  ya kusema

“Ripoti hii ya WHO inatoa matumaini sana,  ukizingatia kwamba katika miaka iliyopita  takribani watoto  milioni  moja walikuwa wakipoteza maisha kwa  malaria leo hii idadi hiyo imepungua hadi kufika nusu ni jambo la kutia  faraja sana” akasema Chembers

Na kuongeza. “ nimetumia muda mwingi Afrika nimeshuhudia watoto wakifariki,  nimejionea  wadi za watoto zilivyokuwa zimejaa huku watoto wakilala wawili katika kitanda kimoja. Lakini leo hii katika baadhi ya nchi wadi za watoto zipo tupu na vitanda vinatumika kwa  huduma nyingine”.
Posted by MROKI On Friday, December 13, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo