Nafasi Ya Matangazo

July 18, 2013

“Happy birthday Mzee Madiba.” Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo ametimiza umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.

Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern Cape na ametumia zaidi ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na usawa wa wananchi wa Afrika Kusini.

Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.

Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.


Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’ ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya kuzaliwa.

Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.

Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.

Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.

Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania haki na utu’.

Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine ambao ni wahitaji katika jamii.

Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo ambaye ni alama ya dunia.

Nchini Tanzania napo jamii imeombwa kufanya matukio kama hayo ya kuisaidia jamii hasa wasio jiweza na watoto yatima kumuenzi kwa vitendo Baba wa Taifa la Afrika Kusini mzee Madiba.

Ofisi za UN Tanzania kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini na Waafrika Kusini waishio Tanzania wameaanda maadhimisho hayo yatakayo fanyika kituo cha Yatima cha St Teresa’s Children’s Home kilichopo Mburahati, Kigogo Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana hii leo. 

Wananchi walio na vitu mbalimbali kama nguo, vyakula, madaftari, vitabu na vitu mbalimbali kwaajili ya kusaidia yatima hao wameombwa waje navyo pamoja na hivyo, shughuli za usafi zitafanyika kituoni hapo. 

Posted by MROKI On Thursday, July 18, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo