Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akipokea tuzo ya Millenium Development Goals, Women Progress Awards,2013, kutoka kwa Ms Jennie Yeung , Rais wa Shirika la Sun Zhong Shan Foundation lililo chini ya United Nations Education, Science, Cultural and Health Advancement Foundation la nchini Marekani. Mama Salma alipokea tuzo hiyo baada ya kutimiza baadhi ya malengo ya Millenia katika masuala ya ukimwi, elimu kwa watoto waliokosa fursa na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini Tanzania. Kulia ni Katibu wa WAMA, Ndugu Daud Nassib na kushoto ni Dr. Judy Kuriansky, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.
***** ******
Na Anna Nkinda – New York
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya
Malengo ya Maendeleo ya Milinia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika la Voices
of African Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa anayoifanya
ya kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.
Sherehe ya kukabidhi tuzo hizo zimefanyika jana
katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Umoja wa Mataifa
(UN) mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi wake
madhubuti, mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia wanawake na
watoto wa Tanzania.
Akikabidhi tuzo hizo Nana – Fosu Randall ambaye ni Rais
na mwanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tathimini ilitofanyika kwa
mwaka 2012 juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia wametambua kwamba malengo
matatu yamefikiwa nchini Tanzania kabla ya muda uliowekwa wa kikomo
wa mwaka 2015.
Alisema kuwa wake wa Marais wa Afrika wanamajukumu
mbalimbali katika nchi zao ili kufikia Malengo hayo, Taasisi ya VAM imekuwa
ikifanya tathimini juu ya hatua zilizofikiwa na Taasisi za wake wa Marais
kupitia taarifa za mwaka na zingine zinazowasilishwa.
“Wanawake hawa wanastahili kutuzwa kwani wamefanya
kazi kubwa pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira yenye changamoto
nyingi ukilinganisha na wenzao katika nchi zingine.
Hafla ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio ya
wake wa marais wa Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati huu
ambapo mwaka 2015 unakaribia”, alisema .
Alimalizia kwa kusema kuwa mara nyingi vyombo vya habari
vimekuwa vikiandika habari zisizokuwa sahihi kutokana na kazi
zinazofanywa na wake wa marais lakini vinasahau kuandika mambo mazuri na kazi
kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia wananchi na kuviomba vyombo hivyo kubadilika
na kuthamini kazi kubwa wanayoifanya.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete
alishukuru kwa tuzo aliyopewa na kusema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo
zimepiga hatua kubwa sana katika kufikia malengo ya milinia kwani vifo vya
watoto vimepungua kwa asilimia 45 na 49 kwa watoto wachanga.
Alisema kuwa haya ni mafanikio makubwa sana japokuwa
lengo ni kuondoa kabisa vifo ambavyo vinatokana na sababu ambazo
zinazuilika na katika malengo mengine maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) yanaendelea kupungua kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1
kwa mwaka 2011.
Mama Kikwete alisema, “Elimu ya msingi inatolewa bure kwa
watoto wote walio na umri unaostahili na hatua kubwa imepigwa katika kupunguza
ugonjwa wa maralia na vifo vya akina mama vinavyotokana na tatizo la uzazi”
Kwa upande wa harakati za kumkomboa mtoto wa kike alisema
kuwa ni lazima ziendelee na zizingatie changamoto mpya za mazingira mapya kwani
unapompatia elimu unampunguzia changamoto za ujinsia na kumpatia huduma ya afya
ikiwemo uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi shughuli za maendeleo ya
kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza kuendelea.
Kwa upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni mwakilishi
wa Asasi zisizo za Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake wa marais
wanafanya kazi kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila mmoja
kuwaunga mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya
maendeleo ya milinia.
Dk. Kuriansky alisema kuwa ili kufikia malengo ya milinia
inatakiwa kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo litasababisha kuifikia
jamii kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.
Tuzo hizo zimetolewa kwa mara ya kwanza na shirika hilo
kwa kushirikiana na Taasisi ya The reed for Hope (RFHF) na Bethesda Counsel kwa
wake wa marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Denice
Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial Guinea Mama Mintou Doucoure Epse
Traore na Mke wa Rais wa Mali Mama Dk. Malika Issoufou.
0 comments:
Post a Comment