Nafasi Ya Matangazo

May 07, 2013

Wakati maofisa wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (FBI) wametua Arusha, raia wanne wa Saudi Arabia na Watanzania wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika kulipua bomu lililoua watu wawili na kujeruhi wengine 61 wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti.

Waliofariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45), mkazi wa Olasiti na James Gabriel (16), ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo lilitokea wakati Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini, Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizindua kanisa hilo.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema raia hao wa Saudi Arabia walikamatwa jana asubuhi baada ya tukio wakiwa kwenye gari wakielekea Kenya kupitia Namanga.

Mulongo alisema raia hao wa kigeni waliingia nchini Jumamosi iliyopita na siku iliyofuata ndipo kukatokea ulipuaji huo. Alisema lengo la shambulizi hilo lilikuwa kumdhuru Askofu Padilla.

“Mtu ambaye tulimkamata jana (juzi Jumapili) ndiye aliyesaidia kuwapata watu hawa wa Saudi Arabia na Watanzania hao,” alisema Mulongo.

Mulongo alisema maofisa wa FBI walifika jana saa tano asubuhi ili kusaidiana na Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika uchunguzi wa tukio hilo.

Maofisa hao wa FBI walikuwa Zanzibar ambako walikuwa wanachunguza kifo cha Padri Evaristus Mushi ambaye aliuawa Februari 17, mwaka huu.

Hii itakuwa mara ya pili kwa wageni kuhusishwa na matukio ya ugaidi nchini baada ya mwaka 1998 wakati raia kadhaa wa Misri wakiongozwa Fazul Abdulla waliposhirikiana na Watanzania kadhaa akiwamo Ahmed Ghailani kulipua ubalozi wa Marekani nchini na ule wa Kenya. Ghailani anatumikia kifungo cha maisha nchini Marekani wakati Fazul aliuawa Somalia mwaka 2011. SOMA zaidi MWANANCHI ONLINE
Posted by MROKI On Tuesday, May 07, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo