Nafasi Ya Matangazo

March 13, 2013

Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana (kushoto) akiwa katika mazungumzo na Kamishna wa maadili na nidhamu wa Chama Cha Kikomunisti cha China (PCP) jimbo la Dongguan, Cui Jian, kwenye hoteli ya Exibition International  mjini Dongguan, China hii leo. Kinana na ujumbe wake wapo nchini China kwa ziara ya siku kumi ya kimafunzo kwa mwaliko wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC).
 ******      ********
Na Bashir Nkoromo.
Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kimeeleza matumaini yake kwamba upo uwezekano wa Tanzania kupiga hatua kubwa kichumi kama itajikita kwa dhati katika kuzitumia rasilimali ilizonazo ikiwemo ardhi.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Maadili na Nidhamu wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), jimbo la Donguan, China,  Cuo Jian, wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na ujumbe wake katika hoteli ya Exhibition Internation.

Jian ambaye pia ni Meya wa jiji la Donguan, amesema, Tanzania kama zilivyo nchi kadhaa za Afrika, inaweza kupiga hatua kiuchumi ikiwekeza juhudi zake katika kuzitumia rasilimali ilizonazo kwa kuwa rasilimali ndiyo msingi wa kwanza katika kuinua uchumi wa nchi yoyote.

Amesema, anatambuwa kwamba Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zenye ardhi kubwa, hivyo haina budi juhudi zake za kuinua uchumi kuzielekeza katika rasilimali hiyo ikiitumia kwa kilimo cha kisasa, kujenga viwanda na vitega uchumi mbalimbali ambavyo vitachochea kukua haraka kwa uchumi.

“Hata hivyo nawapongeza Tanzania, kwa hatua mliyofikia sasa katika kukuza uchumi, asilimia sita ya GDP, inaridhisha, la msingi serikali  kuongeza juhudi na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika juhudi hizo”, amesema, Jian.

Akijibu swali la Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, ambaye yupo kwenye msafara wa Kinana katika ziara hiyo, Titus Kamani aliyetaka kujua ni nini hasa China ilifanya hadi kuufanya uchumi wake ukue haraka na kuwa nchi ya pili dunia kwa maendeleo, Jian amesema, China imefikia mafanikio hayo kutokana na kuamua kuwekeza kwa nguvu zake zote kwenye rasilimali ya ardhi.

“Zipo njia nyingi za kuweza kuinua uchumi wa nchi yoyote, juhudi hizo baadhi zinafanana na nyingine ni tofauti kutokana na nchi na nchi, lakini sisi (Wachina) tulifahamu kwamba tuna ardhi kubwa sana, hivyo tukaamua kutumia rasilimali hii kwa kila namna iliyo bora.  Licha ya eneo kuwa kubwa lakini tumehakikisha hakuna eneo linaloachwa bila faida”, alisema.

Kinana yupo nchini China akiambatana na ujumbe wa viongozi na maofisa wa Chama kwa ajili ya ziara ya mafunzo, katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa, na pia kudumisha urafiki wa kindugu wa siku nyingi kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chama Cha Kikomunisti cha nchi hiyo.

Katika ziara hiyo Kinana amefuatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Khadija Aboud, Katibu wa NEC, Siasa na Uhuaisno wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martine Shigela, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi, Khamis Suleiman Dadi na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi Mohammed Yusuf Mohamed.

Wengine ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa,  Jesca Msambatavangu, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Titus Kamani, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema na maofisa wa Chama. ziara hiyo.

Kinana anafanya ziara  hiyo kutokana na mwaliko wa Chama Cha Kikomunisti cha China, na anafanya ziara hiyo ikiwa ni ya kwanza kuifanya nje ya nchi, tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Oktoba mwaka jana mjini Dodoma.
Posted by MROKI On Wednesday, March 13, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo