Na Anna Nkinda – Magu
Kina mama Wajasiliamali nchini wametakiwa kuongeza
ubunifu katika vikundi vyao ikiwa ni pamoja na kutengeneza bidhaa bora zaidi ambazo zitakidhi kiwango cha kimataifa na hivyo kuwa
na soko la uhakika la ndani na nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wajasiliamali wa mkoa wa Mwanza kwenye
kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke Duniani zilizofanyika katika kituo
cha utamaduni Bujora wilayani Magu.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi
ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) pia aliwataka wanawake hao wajasiriamali kutengeneza mazingira mazuri ya
kufanyia kazi na kutafuta masoko ya
bidhaa zao hasa mayai na vyakula ambayo yanapatikana kirahisi katika mkoa wa
Mwanza na mikoa jirani.
Aliendelea kusema kuwa hivi sasa kina mama wengi
wanaungana na kufanya kazi kwa pamoja katika vikundi vya ujasiriamali hii ni ishara kuwa kila mwanamke anashauku ya
kufanya kazi ya maendeleo bila ya kutegemea msaada wa mwanaume.
Mama Kikwete alisema, “Ninawashukuru kwa kazi
njema mnazozifanya na ninapenda kuwahakikishia kuwa niko nanyi katika
mihangaiko na juhudii zenu zote. Nitajitahidi niwezavyo na kadri Mungu
atakavyonijalia kuwawezesha katika elimu ya ujasiriamali kupitia taasisi ya
WAMA kila itakapowezekana”.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisisitiza kuwa juhudi
za ukombozi wa mwanamke zilianza zamani na mtu mmojammoja. Lakini kwa sasa juhudi
hizi zinapaswa kuenziwa kwa mshikamo na
kuwa wamoja zaidi ili kila mtu kwa nafasi yake aweze kumkomboa mwanamke kielimu na kiuchumi.
Akisoma taarifa ya wanawake wajasiliamali hao Mwadawa
Tofiki alisema kuwa wanajishughulisha na usindikaji wa vyakula, upambaji,
upishi, ufugaji, ufumaji, utegenezaji wa sabuni na batiki, ufinyanzi, uhunzi,
vikoba, uwekaji wa hisa, Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS),sanaa na
burudani.
“Licha ya kujishughulisha na kazi za
ujasiliamali pia tunatoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi, yatima na wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) , wajane,
wazee na watu wenye ulemavu.
Kauli mbiu ya mwaka 2013 ni “Uelewa wa masuala
ya jinsia katika jamii ongeza kasi”, ambayo inaonyesha wazi kwamba sisi
wanawake tunayo majukumu makubwa na muhimu kifamilia na kijamii kama vile kulea
na kushirikiana na wanaume katika shughuli za kijamii na uzalishaji mali”
alisema Tofiki.
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni elimu duni katika masuala ya ujasiliamali na
sheria, ushirikishwaji duni katika masuala ya kkijamii, kiuchumi na kisiasa,
huduma duni ya afya ya mama na mtoto, baadhi ya kina baba kutelekeza familia
zao, wanawake kunyimwa haki ya kulimiliki au kurithi mali.
Ukosefu wa masoko kwa bidhaa za uzalishaji mali
kama vile kilimo cha mbogamboga , ufugaji na usindikaji wa vyakula na matunda,
gharama kubwa za upatikanaji wa pembejeo, wajane na watoto yatima kutokupewa
kipaumbele katika utoaji wa huduma za afya na uporomokaji wa maadili katika
jamii.
Taasisi ya WAMA iliwachangia wanawake hao
wajasiliamali shilingi milioni tano
fedha ambazo watagawana katika vikundi vyao na ziwatasaidia kuinua mitaji yao ili waweze kuwa endelevu katika shughuli zao
za maendeleo.
0 comments:
Post a Comment