Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amewataka waombaji uongozi ambao hawaridhiki na uamuzi wa Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi kutafuta haki yao kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo (Februari 16 mwaka huu) mchana, Rais Tenga amesema TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka kwa wadau wake.
“Wote
tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea wetu
wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu
unaoeleweka. Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo njia za
kufuata.
“Katika
mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine wanaachwa. Wameachwa
kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi. Ambaye
haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu
wa taratibu,” amesema.
Rais
Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia uamuzi
unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia
kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi
waliofikia.
Amesema
ambao hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF
dhidi yao wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda
Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
“Hata
ukiweka ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu. Kwa Katiba yetu
hapa (Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo kingine.
Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote
ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa
maslahi ya mpira wa miguu tutasaidia katika hilo wapate haki,” amesema
Rais Tenga na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa uamuzi wa Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati hiyo
hiyo.
Amesema
TFF imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa
likizungumzwa kinazi zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi
ya mpira wa miguu ni vizuri taratibu zikafuatwa.
“Nawaomba
washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki (TFF) kwa muda
mrefu. Bado tunaomba watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi kubadili
kitu. Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa kutafuta
haki yake.
“Hizi
ni kamati huru, lazima ziheshimiwe. Ukianza kuziingilia utakuwa umeua
mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi, tusionekane tunagombana. Huu si
ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda kulipwa mshahara. Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi,
tulishaondoka huko,” amesema.
Kuhusu
mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya waraka, Rais Tenga
amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri. Maeneo
yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni
maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Amesisitiza
kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na hakuna udanganyifu katika
hilo, kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na Mkutano ni watu ambao
ndiyo wamepitisha mabadiliko hayo.
“Mkutano
Mkuu ni watu, si kikao. Katika dunia ya leo mikutano inafanyika kwa
tele conference, si lazima watu wakutane sehemu moja,” amesema na
kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa kura 70 dhidi ya 33
zilizokataa.
Kuhusu
Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema tarehe ya kuanza
kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri wa
Msajili ulipopigwa. Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana,
Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment