Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2013

 Mratibu wa Kituo cha Mabinti kilichopo chini ya Hospitali ya CCBRT Bi. Katia Geurts  akiwaelezea Maafisa wa Vodacom Foundation  shughuli zinazofanywa na kituo hicho wakati walipotembelea kuona miradi mbalimbalia wanaoyoifadhili ,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu ya Fistula katika Hospital ya CCBRT na Kupona  ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao.
 Mmoja  wasichana  wa kituo cha "Mabinti" aliyepata kutibiwa Fistula na kupona katika Hospitali ya CCBRT Bi. Roida George  akionesha umahiri wa kushona kofia wakati Maafisa wa Vodacom Foundation  ambao ndio wadhamini wa miradi yao walipotembelea katika kituo hicho  kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.Kituo hicho kinawawezesha mabinti hao  kupata elimu ya kazi za mikono  ili waweze kujikimu kimaisha pindi wanaporudi makwao.
Mratibu wa Kituo cha Mabinti kilichopo chini ya Hospitali ya CCBRT Bi. Katia Geurts  akifafanua jambo Maafisa wa Vodacom Foundation jinsi  shughuli zinazofanywa na kituo hicho wakati walipotembelea kuona miradi mbalimbalia wanaoyoifadhili ,Mabinti hao wanapata elimu ya kazi za mikono mara baada ya matibabu ya Fistula katika Hospital ya CCBRT na Kupona  ili waweze kujikimu kimaisha wakati wanaporudi makwao,wapili toka kuliani Meneja wa Vodacom Foundation Grace Lyon,Afisa wa Vodacom Foundation Ally Mbuyu na Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania Bw.Matina Nkurlu.
*********
Wanawake waliougua  kutibiwa na hatimaye kupona maradhi ya fistula katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam wameamua kujikita katika sanaa ya kazi za mikono kwa lengo la kujiajiri sambamba na kujikwamua na wimbi la umasikini.

Takribani wanawake wapatao 62, chini ya mpango madhubuti ulioratibiwa na hospitali ya CCBRT, wamekuwa wakihitimu mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono zikiwemo sanaa za ushonaji wa batiki, nguo za aina tofauti, utengenezaji wa mabegi, kofia, ususi na kadhalika, katika Kituo kinachoendeshwa na hospitali hiyo kijulikanacho kama 'Mabinti' tangu mwaka 2007.

Akizungumza mbele ya ujumbe wa wadhamini waliotembelea kituo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mratibu wa Kituo hicho, Katia Geurts, alisema kituo hicho kinatoa mafunzo mahsusi kwa wakinamama waliopona baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa fistula. "Wengi wao wanatoka katika familia duni, hivyo mafunzo haya wanayoyapata baada ya kumaliza matibabu ya Fistula yanakwenda kuwasaidia kujiajiri wao wenyewe jambo linalowasaidia kupunguza ukali wa maisha," alisema Geurts.

Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo kituo hicho huwapatia vyeti vya uhitimu vinavyotambulika, sanjari na vitendea kazi vinavyoendana na stadi stahiki aliyohitimu mwanafunzi kwa minajiri ya kuwarahisishia upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha yao.

Nae Mkufunzi wa Kituo hicho ambaye awali alikuwa mmoja wa waathirika wa ugonjwa wa fistula hospitalini hapo, Jane Rugalabamu, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aanze kufundisha wenzake kituoni hapo amebaini kuna idadi kubwa ya wanawake wenye matatizo ya fistula ndani ya jamii lakini waume zao wamekuwa wakiwaficha kwa dhana ya kufisha aibu.

"Kuna haja kubwa ya kuelimisha akinababa wawaruhusu wake zao wenye matatizo waje kutibiwa. Ugonjwa huu unatibika na wala sio wa kurogwa kama wengi wanavyodhani, sisi sote hapa kwenye kituo cha mabinti tulikuwa na maradhi hayo na sasa tumepona kabisa wanawake jitokezeni," alisema Rugalabamu.

Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha Vodacom  Foundation, Grace Lyon,  baada ya kukagua shughuli mbalimbali za mafunzo zinazoendelea kituoni hapo, alisema kwa niaba ya wafanyakazi wa Vodacom na Vodafone duniani kote, wataendelea kuwasaidia akinamama wote wanaopatwa na maradhi ya fistula hatua kwa hatua, sanjari na kuhakikisha wanazidisha kasi katika kampeni inayoendelea dhidi ya maradhi hayo.

"Tutaendelea kuwa karibu zaidi na waathirika wa fistula kuanzia hatua ya kuwasafirisha kutoka vijijini na mikoani kwa kuwatumia fedha kupitia huduma yetu ya M-Pesa, pia tutakuwa pamoja wakati wote wa matibabu na baada ya kupona tutawaunga mkono kwenye mafunzo kama haya ili kuwaletea ustawi ulio bora kwa maisha bora kwa ajili yao na familia zao," alisema Lyon.
Posted by MROKI On Sunday, January 27, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo