Na Baltazar Nduwayezu,EANA
Zaidi
ya watu 1,000 kutoka Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani wanatarajiwa
kuhudhuria mkutano wa wa siku tatu wa Nishati ya Petroli na Maonyesho
utakaofanyika mjini Arusha, kati ya Februari 6 na 8, 2013.
‘’Lengo kuu la Mkutano na Maonyesho ni
kukuza uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuionyesha dunia rasilimali
ya nishati hiyo iliyopo katika kanda na kubadilishana taarifa juu ya hali ya
uendelezaji wa sekta hiyo katika kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC),’’ Dk. Nyamajeje Weggoro,Mkurugenzi wa Tija na
Sekta ya Jamii wa EAC aliwaambia waandishi wa habari hapa juzi.
Aliongeza kwamba mkutano huo utatoa
mada mbalimbali za kiufundi zinazoonyesha maendeleo ya sekta ya mafuta
ya petrol na gesi katika EAC na duniani kwa ujumla
wake.
‘’Hii ni nafasi ya kipekee kwa Afrika
Mashariki kuonyesha ugunduzi wa hivi karibuni wa uwepo wa mafuta na gesi na
kuona ni namna gani bora ya kuweza kuchimba rasilimali hiyo katika nchi
wananchama,’’ alisema Dk. Weggoro. Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na
Rais Jakaya Kikwete.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni : ‘’Kanda ya
Afrika Mashariki,eneo linaloibukia kwa uwekezaji na upatikanaji wa mafuta na
gesi kwa siku za usoni kwa maendeleo endelevu.
‘’Tumechagua kauli mbiu hiyo kwa sababu
upo ugunduzi mkubwa wa mafuta na gesi katika miaka miwili iliyopita Magharibu
mwa Uganda na katika maeneo mengine,ugunduzi wa gesi Kusini mwa Tanzania na
ukanda wa Pwani, ugunduzi mkubwa wa mafuta Kaskazini mwa Kenya na gesi pia
ukanda wa Pwani wa Kenya,’’ alieleza Dk. Weggoro na kuongeza ‘’hali hii
imeifanya kanda hii kuwa na mvuto wa aina yake kwa wawekezaji kutoka duniani
kote.’’
Wajumbe waliothibitisha kushiriki
katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa biashara katika sekta ya
nishati,mawaziri wa shughuli za EAC, mawaziri wanaoshughulikia nishati, fedha na
mipango toka nchi tano za EAC na sekta nyingine muhimu,
wawakilishi toka sekta binafsi, bodi mbalimbali za kitaaluma, vyuo vikuu na
kampuni kubwa za uchimbaji petroli na gesi.
Mkutano huo wa Afrika Mashariki wa
Nishati ya Petroli unaofanyika kila baada ya miaka miwili ulizinduliwa rasmi
mwaka 2003 na unafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama.
0 comments:
Post a Comment