Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wapya wa Chama cha
Netiboli Mkoa wa Dar es Salaam (CHANEDA), wanatarajiwa kutambulishwa Ijumaa
katika tukio litakalohusisha mechi kadhaa za netiboli baina ya timu zilizopo
mkoani humo.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano na
Mawasiliano wa CHANEDA, Michael Maurus, utambulisho huo utaanza saa nane mchana
kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Alizitaja timu zitakazopambana
katika utambulisho huo kuwa ni Kaza Roho ya Kiwalani na Majumba Sita ya Ukonga
(wanaume), huku pia zikiwamo timu za watoto ambazo ni Kiwalani Kids na Ukonga
Kids.
“Kwa upande wa timu za wanawake,
zilizothibitisha kushiriki ni Uhamiaji, Bandari Queens A, Bandari Queens B, CBE
na Chuo Kikuu cha Tumaini,” alisema Maurus.
Aliwataja viongozi
watakaotambulishwa siku hiyo baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita kuwa
ni
Winfrida Emmanuel (Mwenyekiti), Pili
Mogella (Makamu Mwenyekiti), Joseph Ng’anza (Katibu Mkuu), Christina Kimamla
(Katibu Msaidizi), Anitha Lunogela (Mhazini) na Maurus.
Maurus aliwataja wajumbe kuwa ni Khadija
Ally, Zainab Seif, Georgina Kasembe na
Mussa Sambala ambapo aliwataka wadau wa netiboli na
michezo kwa ujumla jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku hiyo
kuwafahamu viongozi wao, lakini pia kushuhudia mechi hizo.
0 comments:
Post a Comment