JESHI la
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo, imemtia
mbaroni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam,Sheikh Issa Ponda Issa.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi kanda maalum,Suleiman Kova,
alisema kuwa Ponda amekamatwa kutokana na kukabiliwa na tuhuma
mbalimbali ikiwemo uchochezi dhidi ya Serikali iliyoko madarakani.
Makosa
mengine ni uchochezi wa udini kati ya waislamu na wakristo na ndani ya
waislamu wenyewe,kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani jijini.
Tuhuma
nyingine ni kulazimisha watu kufanya maandamano hasa wanawake na
watoto,kumtisha kumuua sheikh Mkuu Mufti Issa Shaaban bin Simba,
kujisifia kuingia Makao Makuu ya Jeshi la Polisi bila ruhusa na uvamizi
wa kiwanja.
Tuhuma
nyingine ni kuingilia uhuru wa Mahakama, umwagaji wa damu, uchomaji wa
makanisa zaidi ya nane, uharibifu wa magari, wizi, upotevu wa vifaa vya
makanisa. “Sheikh ponda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya
dola na kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai watuhumiwa waliokamatwa
kwa uvunjaji wa makanisa na kufikishwa Mahakamani waachiwe mara moja
kabla ya siku saba”alisema.
Ponda alikamatwa juzi majira ya saa 4:30 usiku akiwa kwenye pikipiki kuelekea katika maficho yake maeneo ya Temeke.
“Juzi
usiku sijalala kabisa kuhakikisha oparesheni ya kumkamata inakwenda
salama, Ponda ni mjanja sana ila Serikali ina mkono mrefu kabla ajaingia
katika maficho yake Temeke,alijaribu kukimbia ili atoroke lakini
akakamatwa”alisema.
Kova pia
alisema kuwa mnamo Oktoba 12,mwaka huu Ponda aliwaongoza wafuasi wake
na kuvamia kiwanja namba 311/2/4 block T chang’ombe mali ya kampuni ya
Agritanza kwa madai ya kulikomboa.
“Ponda
akiwa na wafuasi wake walivamia kiwanja hicho cha agritanza na kudai
kuwa wanakomboa mali za waislamu zilizouzwa na Bakwata,uchunguzi wa
awali unaonyesha kuwa kiwanja hicho kina hati miliki namba 93773
iliyotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na mikataba mbalimbali ya
kuuziana”alisema
Aidha
Kova alisema kuwa uongozi wa Bakwata ulipeleka mashahidi kuthibitisha
uhalali wa kiwanja hicho na kusema kuwa watu waliovamia wanakabiliwa na
shitaka la kuingia kwa jinai pamoja na uharibifu wa mali.
“kati ya
watu 38 tuliowakamta wanawake ni saba na wanaume ni 31 na tuliwakuta na
silaha mbalimbali kama visu,mapanga,sururu na vifaa vya kuvunjia na vya
ujenzi,jenereta na kujenga jengo la haraka”alisema Kova.
Aidha
Jeshi la Polisi limesema kuwa limemvumilia Ponda kwa muda mrefu na
kuwataka watu wanaoandamana kinyume cha taratib kuacha. “Nawasifu sana
wakristo ni wavumilivu,wanabusara kwa tukio la mbagala la kuchoma
makanisa la sivyo hali ingekuwa ya hatari na hata hivyo Jumuiya ya
Taasisi za Kiislamu haijasajiliwa kisheria”alisema.
Kova
amewataka wafuasi wengine wajisalimishe kwani oparesheni inaendelea na
watawachukulia hatua za kisheria. Pia amewaasa wananchi kutumia akili
zao binafsi na kuacha kufuata mkumbo watashughulikiwa.Jeshi la Polisi
linatarajia kumfikisha Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Moto
ukiwaka eneo la Darajani mjini Unguja, Zanzibar jana, kufuatia vurugu
kubwa zilizoanzishwa na wafuasi wa kikundi cha kidini cha Uamsho
wakipinga kile kilichozagaa kuwa ni kukamatwa kwa kiongozi wa kikundi
hicho, Sheikh Farid. (Picha kwa hisani ya Wavuti.com)
0 comments:
Post a Comment