Na Mwandishi Wetu
KATIKA
kuhakikisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
anaenziwa kipekee, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaendesha
zoezi la upimaji afya za wanachama na wananchi kwa ujumla mkoani
Shinyanga ambako kilele cha maadhimisho hayo yatafanyika Oktoba 14,
mwaka huu.
Akizungumzia
zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji Eugen Mikongoti alisema kuwa,
Mfuko umefikia uamuzi huo kwa lengo la kuenzi mazuri yote yaliyofanywa
na Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
“Baba wa
Taifa aliapa kupigana na maadui watatu ambao ni Umasikini, Ujinga na
Maradhi na katika hayo sisi ni wadau wakubwa katika kupambana na adui
maradhi na ndio maana tumeona tumuenzi kwa njia hii ambapo wananchi
watapima afya zao bila malipo na kupata ushauri wa kitaalam ili
kuepukana na maradhi yasiyoambukiza,” alisema Mikongoti.
Mbali na
upimaji wa afya kwa wananchi, alisema kuwa Mfuko unatumia fursa hiyo
kujibu kero mbalimbali za wanachama wake ambao watafika katika viwanja
vya Sabasaba ambako Mfuko umeweka banda kwa ajili ya kuendesha zoezi la
upimaji na utoaji wa elimu juu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na
Mfuko wa Afya ya Jamii, kwa muda wa siku tano, kuanzia jana.
Alisema
kuwa lengo kubwa la NHIF ni kuhakikisha wanachama wake na wananchi kwa
ujumla wanapata huduma bora za matibabu na Vituo vya kutolea huduma hizo
vinaboreshwa kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi kupitia fursa
inayotolewa na Mfuko huo ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa
majengo.
“Mfuko
umekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma za afya vituoni
zinakuwa bora na unafanya hivyo kwa kutambua kuwa mhimili mkubwa wa
Mtanzania katika kufanya kazi na kujiondolea umasikini ni afya yake
kwanza…nawaomba wananchi wa Shinyanga na wa maeneo mengine mfike katika
banda letu ambalo linatoa huduma za upimaji na elimu ya afya kwa
ujumla,” alisema.
Mikongoti
alisema kuwa Mfuko utaendelea kumuenzi Baba wa Taifa katika kupambana
na adui maradhi kwa kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa
matibabu kupitia utaratibu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
na Mfuko wa Afya ya Jamii.
Wakati
huo huo, Mfuko umeendelea na jitihada zake za kuhakikisha makundi maalum
yanapata huduma bora baada ya kuchangia jumla ya shilingi milioni 1.5,
shuka 80 na fulana 80 kwa Kituo cha Mihuji Chesire Home kilichopo mjini
Dodoma ambacho kinalea watoto wenye matatizo ya mtindio wa ubongo.
Mchango
huo wa NHIF ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma katika
harambee ya kuchangia kituo hicho na Meneja wa Kanda ya Kati Dkt. Daudi
Bunyinyiga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Emanuel
Humba.
Akiwasilisha mchango huo, Dokta
Bunyinyiga alisema kuwa Mfuko kama Taasisi inayofanya kazi na Jamii
inawajibu wa kuhakikisha jamii inayoizunguka hususani watu wenye
mahitaji maalum wanafaidika na huduma zake.
0 comments:
Post a Comment