Afisa michezo wa Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba(kulia) akimkabidhi jezi mmoja ya wachezaji wa mchezo wa Pool Mkoani Mbeya wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa vilabu shiriki vya mashindano ya Safari Pool taifa ngazi ya Mkoa.
***** **** ******
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
WADAU wa mchezo wa Pool wametakiwa kuandaa viwanja vingine vya mchezo huo nje ya kumbi za baa ili kutoa fursa ya watoto kujifunza na kuuelewa mchezo huo.
Wito huo umetolewa na jana na Afisa michezo wa Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba wakati akikabidhi vifaa vya mchezo huo kwa ajili ya mashindano maalum ya kukuza mchezo huo mkoani hapa ambayo yamedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Mwakifwamba alisema kuwa licha ya mchezo wa pool hivi sasa unawapenzi wengi na umeendelea kujizolea umaarufa katika maeneo mengi nchini, viwanja vingi vya mchezo huo vipo kwenye kumbi za mabaa, hivyo sio vema watoto wakashirikishwa ili kulinda maadili ya taifa.
Alisema kuwa ili kuibua vipaji na kuendeleza mchezo huo kwa vijana wadogo, ni busara kuanza kuandaa viwanja vingine nje ya kumbi za mabaa kwa ajili ya matumizi ya vijana na watoto.
“Mchezo wa Pool umeanza kuwa maarufu nchini na kwa muda mfupi umejizolea wapenzi wengi, lakini changamoto kubwa iliyopo ni viwanja vingi kuwa ndani ya mabaa, natoa wito kwa wadau wa mchezo huu kuandaa viwanja vya watoto ili kuendeleza mchezo huu,” alisema Mwakifwamba.
Mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Septemba 6 mwaka huu yanatarajia kufikia kilele chake Septemba 10, mwaka huu katika ukumbi Blue House eneo la Kabwe Jijini Mbeya yakishirikisha timu tisa kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya.
Pia Mwakifwamba alizitaka timu zinazoshiriki mchezo huo kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kukubali matokeo hata pale zinapokuwa zimeshindwa na wapinzani wao.
Meneja matukio wa TBL Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Francis Mwasamwene, alisema kuwa lengo la TBL kudhamini mashindano hayo ni kuibua vipaji vya wachezaji wa mchezo huo mkoani Mbeya, na kuviendeleza.
Mwasamwene alitoa wito kwa wachezaji wengi zaidi wenye mapenzi na mchezo huo kujitokeza kushiriki mashindano hayo kwa kuwa hadi sasa kuna jumla ya timu tisa tu zinazojulikana mkoani Mbeya.
“Tunahitaji kuona mchezo huu ukiwa na timu nyingi zaidi mkoani hapa na hili litafanikiwa zaidi kwa timu nyingi zaidi kujisajili, TBL imeamua kudhamini mashindano haya ili kuweza kuibua vipaji vya wachezaji wa mchezo huu,”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mchezo wa Pool mkoani Mbeya, Obeidy Malabeja, alisema mchezo huo ni kama ilivyo michezo mingine na unaendeshwa kwa sheria zake halali zinazoulinda.
Malabeja alizitaja timu zitakazoshiriki mashindano hayo kuwa ni Container ya Tunduma wilayani Momba, Nakonde, Lunch Time ya Mbozi, Kizota, Royal Zambezi, Blue House, Shooters, Royal Class na Stendi Kuu ya mabasi mkoani Mbeya.
Vifaa vilivyotolewa na TBL na kukabidhiwa kwa timu hizo na Afisa Michezo wa Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba ni pamoja na Jezi seti moja pamoja na simu ya mkononi kwa kila timu inayoshiriki mashindano hayo.
0 comments:
Post a Comment