Nafasi Ya Matangazo

September 07, 2012

Takriban watu kumi na moja wa kabila la Pokomo wameuawa katika mashambulizi mapya ya kulipiza kisasi katika eneo la Tana River,Kusini Mashariki mwa Kenya.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema alisikia watu wakipiga mayowe wakati kijiji kimoja kilipokuwa kinashambuliwa na kisha wenyeji kuteketezwa.Eneo hilo ambako zinaishi jamii za kuhamahama ni kitovu cha mizozo ya ardhi na maji kati ya jamii za Orma na Pokomo.

Watu wengine kumi walijeruhiwa kwenye uvamizi huo uliotokea usiku wa kuamkia leo.

Uvamizi huu umetokea baada ya mashambulizi mengine kutokea mwezi jana ambapo watu 52 kutoka jamii ya Orma wengi wakiwa watoto na wanawake kuuawa kwa kunyongwa na kuteketezwa kiasi cha kutotambulika.

Ni katika tukio ambalo lilitajwa kuwa ghasia mbaya za kikabila kutokea katika miaka ya hivi karibuni nchini Kenya. Polisi na viongozi wa kijamii walisaidia kutuliza hali na kurejesha usalama kati ya jamii hizo mbili lakini hali ya wasiwasi iimeendelea kutanda.

Licha ya kwamba polisi waliahidi kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo, viongozi wa eneo hilo wanasema vikosi vya usalama vimeshindwa kuzuia ghasia.

Mbunge wa eneo hilo, Danson Mungatana amewashtumu maafisa wa usalama kwa kushindwa kuchukua hatua za kuwalinda wananchi licha ya kufahamu mapema kwamba mashambulio yatatokea.

Jamii hizo mbili za Pokomo na Orma, zimekuwa zikizozana kuhusu matumizi ya ardhi na maji ambazo ni rasilimali adimu.

Wapokomo ni wakulima ambao hukuza chakula kando ya mto Tana wakati jamii ya Orma wakiwa wafugaji wa kuhamahama.

Chanzo: http://www.bbc.co.uk/swahili/habari
Posted by MROKI On Friday, September 07, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo