Picha: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw, Zelothe Stephen, Kulia akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi kuhusu Vifo vya wahamiaji Haramu Raia wa Ethiopia, Kushoto akisikiliza ni Mkuu wa polisi Wilaya ya Kongwa Bw. Davis Nyanda.
Na. Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limewakamata wahamiaji haramu Themanini na Mbili (82) wote wanaume wenye asili ya Ethiopia jana majira ya 08:OOHRS asubuhi baada ya kuonekana wakitanga tanga katika vijijji vya Chitego na Mkoka Tarafa ya ZOISA Wilayani Kongwa mjini hapa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma. Bw. Zelothe Stephen kuhusu vifo vya Wahamiaji Haramu arobaini na tatu (43) vilivyotokea jana mjini humo alisema Raia hao wote wanatoka Kanda ya Kusini nchini Ethiopia kwenye vijiji vya Kambata, Hadia na Sirite.
Alisema Kukamatwa watu hao walioingia nchini bila kibali kupitia mpaka wa Tanznia na Kenya wakielekea nchini Malawi kulifanikwa baada ya wananchi wema kuwaona na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambapo walifika na kufanya Operesheni Maalum ya Kuwasaka na kuwakamata.
”Wananchi kutoka vijiji hivyo ambavyo vipo umbali wa kilometa 141 toka Dodoma mjini waliweza kuona maiti nyingi zimetupwa kando ya barabara ya Kiteto – Dodoma na baadaye kuwaona watu wengine walio hai katika harakati za kupita Porini kuelekea kijiji cha Izava Wilayani Chamwino hivyo kuingiwa na hofu na kutoa taarifa hizo.”aliongeza Kamanda Zelothe.
Alisema baada ya kupata Taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilifika katika eneo hilo ambako walishirikiana na wananchi wa eneo hilo, hadi kufikia jioni hiyo walifanikiwa kuwakamata raia hao wa Ethiopia wapatao 82 ambao walikuwa wakizungumza lugha ya kiingereza cha kubabaisha.
Kamanda Zelothe Stephen alisema kwa mujibu ya maelezo ya raia hao walisema kwamba walianza safari yao takribani miezi mitano iliyopita wakitokea Ethiopia kuelekea nchini Malawi, kupitia nchini Kenya ambako walidai kuwa ndiko kituo kikubwa cha wao kukusanywa na kuanza safari ya pamoja.
”Walipofika Arusha walitawanywa katika vikundi vidogo na kuhifadhiwa kwenye nyumba mbalimbali huku wakipewa chakula kidogo na maji na kwamba siku ambayo hawakumbuki walikusanywa usiku na kupakiwa kwenye lori moja lililofunikwa kote na kuanza safari kuelekea Malawi.” alisistiza Bw. Zelothe
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Mkoani Dodoma alisema kuwa raia hao wakiwa njiani baadhi yao walianza kuzirai na kufariki, hivyo walifanya jitihada za kupiga kelele na kumgongea dereva lakini hakuwa tayari kusimama hadi walipokuja kutelekezwa usiku wa manane kwenye eneo la tukio hilo na lori hilo kutoweka.
Akizungumzia Hali za maiti katika eneo zilipotupwa, alisema maiti nyingi zilionekana zikiwa tayari zimeanza kuharibika ambapo jumla ya maiti (22 ) zilisafirishwa kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na nyingine (21) zimehifadhiwa kwenye Hospitali ya Serikali Mkoa wa Dodoma kusubiri uchughuzi wa Daktari na taratibu.
Wakati huo huo Kamanda Zelothe amesema huduma za kibinadamu zimekuwa zikitolewa kwa raia hao wa kigeni, na mahali waipohifadhiwa ni jirani na kituo cha Polisi Kati Mkoani Dodoma kwa ushirikiano na taasisi nyingine ikiwa ni pamoja na Idara ya Afya, Red Cross, Uhamiaji na Uongozi wa Mkoa.
Kamanda Zelothe Stephen aliwashukuru wananchi wa Vijiji vya Chitego na Mkoka kwa kutekeleza zana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kwa kutoa taarifa za tukio hilo, aidha wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa za matukio mbalimbali wasiyoyaelewa katika kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi za Kijiji, Kata, Tarafa. Wilaya na Serikali Kuu ili kuweza kudhibiti uhalifu katika maeneo yetu.
0 comments:
Post a Comment