SHUGHULI za uchimbaji wa madini ya Jasi katika vijiji vya Ruvu Jiungeni na Makanya, wilayani Same mkoani Kilimanjaro, zimeendelea kushika kasi huku wachimbaji wadogo wenye leseni zaidi ya 200 wakiungana kuimarisha uzalishaji na usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu kwa viwanda vya saruji na bidhaa nyingine za viwandani.
Wachimbaji hao wameanzisha chama chao kwa lengo la kusimamia maslahi na kuratibu uendeshaji wa shughuli za uchimbaji, hatua inayotajwa kuongeza tija, uwajibikaji na mchango wa sekta hiyo kwa wanachama pamoja na jamii inayowazunguka. Katika kipindi cha takribani mwaka mmoja, wamefanikiwa kuweka mifumo ya pamoja ya usimamizi na udhibiti wa mapato.
Akizungumza wilayani humo, Mhandisi Abel Madaha, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro anayesimamia wilaya za Same, Mwanga, Hai, Rombo, Siha na Moshi, amesema pamoja na fursa za kiuchumi zinazotokana na madini hayo, sheria inazitaka leseni zote kuhakikisha kunakuwa na urejeshaji wa mazingira mara baada ya uchimbaji kukoma.
Amesema kwa kutambua wajibu huo, wachimbaji wameanzisha mfuko maalum wa Ukarabati wa Mazingira (Rehabilitation Fund) wenye akaunti ya pamoja, ambapo kila gari la madini linalotoka eneo la uchimbaji linachangia kiasi maalum cha fedha kwa ajili ya kurekebisha maeneo yaliyoathirika, badala ya kumwachia mchimbaji mmoja mmoja jukumu hilo.
“Mfuko huu unasimamiwa kwa pamoja chini ya Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” amesema Mhandisi Madaha.
Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya madini ya Jasi badala ya kutegemea soko la viwanda vya saruji pekee, akieleza kuwa madini hayo yanaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo gypsum powder, gypsum board, mikanda zinazotumika katika ujenzi na bidhaa nyingine kama chaki nk.
Kwa mujibu wa Mhandisi Madaha, Mkoa wa Kilimanjaro umejipanga kukusanya Shilingi bilioni 4.2 katika mwaka wa fedha 2025/2026 na tayari umevuka zaidi ya asilimia 60 ya lengo hilo, huku madini ya Jasi yakichangia kati ya asilimia 45 hadi 50 ya mapato yote ya Sekta ya Madini mkoani humo.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, jumla ya Shilingi bilioni 2.6 zimekusanywa kutoka shughuli za uchimbaji wa Jasi, jambo linalodhihirisha ukuaji wa sekta hiyo na mchango wake kwa mapato ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Jasi Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Mbwambo, amesema lengo la chama hicho ni kuwaunganisha wachimbaji wadogo, kuongeza uzalishaji na faida, pamoja na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Amesema chama kimeweka mkakati wa kuwa na kiwanda chao wenyewe kitakachotengeneza bidhaa zinazotokana na jasi na kuomba Serikali kuwaunga mkono ili waweze kufikia malengo yao.
Ameongea kuwa chama hicho pia kimejikita katika utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwamo kuchangia huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya uchimbaji, hatua inayolenga kuimarisha mahusiano mema kati ya wachimbaji na jamii.











0 comments:
Post a Comment