Nafasi Ya Matangazo

May 06, 2012

Ndugu zangu,

Kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna  watakaodhani,  kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga  yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote  yule, bila kujali dini, rangi,  itikadi au hata wadhifa wake, anaweza  kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa,  kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa  na wanaowatuma.

Na kwa vyama vya siasa vilivyo makini na  vinavyoitakia mema nchi yetu, vianze sasa kuachana na utamaduni wa kuwa  na ‘wanamgambo’ ama vikundi vya vijana vinavyopewa mafunzo ya kijeshi  kwa masuala ya ulinzi.

Historia inatufundisha,kuwa Afrika  ‘  Parties militias’ ama vikundi vya wanamgambo vya vyama vya siasa huwa  chanzo cha kuharakisha vurugu  za kisiasa za wenyewe kwa wenyewe katika  nchi  na hata kupelekea mauaji. Tumeona Rwanda, Burundi, Jamhuri ya  Kongo na kwengineko Afrika.

Ni vikundi hivi vya wanamgambo wa  vyama ambavyo hutumika na vyama, wanasiasa, au hujituma vyenyewe kufanya  kazi ya kulipiza visasi vya kisiasa kwa kutumia silaha.

Hapa  kwetu tayari, vyama vikubwa vya siasa vina vikundi vya aina hiyo; CCM  wana ‘ Green Guards’, Chadema wana ‘ Red Brigade’ na CUF wana ‘ Blue  Guards’.

Katika nchi ya kisasa si  busara kuwa na utaratibu  unaoruhusu  vyama vya siasa kuwa na vikundi kama hivyo vya vijana vyenye  kupata mafunzo ya kijeshi.

 Na hakika, Katiba yetu ijayo  itusaidie kuondoa utaratibu kama huo wa ‘ kijima’ kwa kuweka marufuku ya  vyama vya siasa kuunda vikosi vya vijana vyenye kukaa kambini na kupata  mafunzo ya kijeshi, vikosi ambayo, vinaweza kuja kutumika vibaya na  kutusababishia madhara makubwa kama taifa.

Kama  vyama  vitahitaji ulinzi kwenye shughuli zake, basi,  viombe ulinzi kwenye  makampuni ya ulinzi yanayotambulika kisheria na yasiyofungamana na siasa  za vyama.

Vinginevyo, tuhakikishe jeshi letu la polisi  linaimarishwa na linakuwa chombo cha usalama kinachoaminika na umma na  kisichoegemea kwenye itikadi za vyama katika kufanya kazi yake. Vivyo  hivyo, kwa vyombo vingine vya usalama katika nchi ikiwamo Idara ya  Usalama wa Taifa.  Vifanye kazi zao kwa kutanguliza maslahi ya taifa na  si ya wanasiasa au vyama vyao. Inawezekana.

( Hii ni sehemu ya makala yangu kwenye gazeti la Mwananchi leo Jumapili)
Posted by MROKI On Sunday, May 06, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo