
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Mageza S. Mulongo kufuatia vifo vya wanafunzi wanane wa Shule ya Msingi Piyaya wilayani Ngorongoro katika Mkoa wa Arusha.
Wanafunzi hao walipoteza maisha Jumatatu tarehe 27 Februari, 2012 wakati wakijaribu kuvuka Mto Losukutane uliokuwa umefurika kufuatia mvua kubwa zilizonyesha katika sehemu mbalimbali za Wilaya ya Ngorongoro jioni ya siku hiyo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za vifo vya wanafunzi 10 wa Shule ya Msingi Piyaya wilayani Ngorongoro katika Mkoa wako wa Arusha waliosombwa na mafuriko ya Mto Losukutane wakati wakijaribu kuvuka Mto huo”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake, na kuongeza, “nimesikitishwa zaidi na taarifa kuwa familia mojawapo katika hizo imepoteza watoto watatu kwa mpigo katika tukio hilo”.
Rais Kikwete amesema tukio hilo limeinyang’anya nchi yetu hazina muhimu ya wasomi wa baadaye ambao hapana shaka Taifa letu lilikuwa linawategemea sana kwa maendeleo yake ya baadaye.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bwana Mulongo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizofikwa na msiba huo.
Akiwahakikishia familia hizo kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao, na amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza vifo vya wapendwa wao.
“Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema azilaze mahali pema peponi roho za wanafunzi wote waliopoteza maisha yao kutokana na mafuriko ya Mto Losukutane”, amemalizia salamu zake za rambirambi Rais Kikwete.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
01 Machi, 2012




0 comments:
Post a Comment