Mwenyekiti wa Gymkhana Golf Club, Dioniz Malinzi, akizungumza katika hafla ya kuiaga timu hiyo, iliyokuwa ikielekea Afrika Kusini kwa michezo ya kujiimarisha, ambayo itakamilika siku ya Jumapili kwa kucheza na timu mbalimbali za huko. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Precision Air, wadhamini wa safari hiyo, Alfonse Kioko.
__________________________________________________________________________________
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Precision Air hivi karibuni imekuwa mstari wa mbele katika kukuza michezo mbalimbali hapa nchini na kwamba imedhamiria kuendelea kuisaidia sekta hiyo ya michezo lengo likiwa ni kuipererusha vema bendera ya nchi yetu katika anga ya kimataifa.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa hafla ya kuiaga timu ya Golf ya Gymkhana kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Alfonse Kioko anasema kwamba kampuni yake imedhaminiria kukuza michezo.
Timu hiyo ilikuwa inakwenda nchini Afrika Kusini kwa mechi mbalimbali za kirafiki na zira hiyo ilikuwa ni ya siku tatu, Precision Air ndiyo walioidhamini safari hiyo kwa upande wa tiketi za safari.
“Tumedhamiria kukuza na kuendeleza michezo hapa nchini, na kwa kweli mkakati wetu huu ni endelevu, “ anasema Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo anaishukuru timu hiyo kwa kuamua kuwa mshirika wa kampuni yake na kuihakikishia kuwa kampuni yake itaendelea kuudhamini mchezo huo wa Golf.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa, Dioniz Malinzi anaipongeza Percision Air kwa udhamini wake wa safari hiyo.
Anasema kwamba udhamini huo utaiwezesha timu hiyo ya golf kwenda nchini Afrika Kusini na kuiperusha vyema bendera ya Tanzania na kuyaomba makampuni mengine kuwa na moyo kama huo.
“Kwa kweli nachukua fursa hii kuipongeza kampuni hii kwa moyo wake wa kizalendo katika kuhakikisha kwamba michezo inakua hapa nchini”
Alisema hivi karibuni kampuni hiyo iliidhamini timu ya Taifa ya Soka ya anawake wakati wa mechi yake nchini Namibia na kwamba udhamini huo ulikuwa ni chachu ya timu hiyo kufanya vema na hatimaye kuipererusha vyema bendera ya Tanzania.
“Udhamini wenu kwenye mechi ya Twiga Stars kwa kweli umelipa, kwa niaba ya Baraza la Michezo la Taifa(BMT), ninapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza sana kwa moyo wenu huo wa kizalendo,”
Mbali na Malinzi, wadau mbalimbali wa Soka hapa nchi wameeleza kufurahishwa na ushiriki wa Precision katika kuisaidia timu ya Twiga Stars.
Dk.Said Ngozi, yeye ni mdau wa soka na mkazi wa, Mazizini,Ukonga Mombasa, Jijini Dar es Salaam, anaipongeza Precison Air kwa kuidhamini timu hiyo ya wanawake ambayo ilikuwa katika hali ngumu kutokana na ukata unaolikabili Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF).
“Hebu fikiria, kama isingelikuwa ni udhamini wa Precision Air, vijana hawa wangekwendaje nchini Namibia, nadhani huu ni mfano kwa kuigwa na makampuni mengine,”
Anasema kwamba kwa kuwa timu zetu zinapofanya vizuri heshima huwa ni kwa Watanzania wote basi Watanzania wenye uwezo hawana budi kushirikiana na vyama vetu vya michezo katika kuhakikisha kwamba timu zetu zinasaidiwa.
“Mimi naamini kwamba kuna Watanzania wengi sana wenye uwezo, nawashauri kutoa ni moyo na si utajiri, basi kwa kuwa bado timu yetu ya Twiga Stars inasafari ndefu, hatuna budi kuisaidia ili iweze kuliwakilisha vema taifa letu, kwanza ndiyo timu pekee ya soka kwa ngazi ya kitaifa inayofanya vizuri,” anafafanua.
Anabainisha kwamba wanawake wanaweza hata kama hawajawezeshwa na kwamba kama wakiwezesha basi wanafanya miujiza ya hali ya juu.
Benjamini Haule, ni mkazi wa hapa Jijini Dar es Salaam, kwa upande wake naye anaipongeza kampuni ya Precision Air kwa kuidhamini timu hiyo ya wanawake na kuiomba iendelee kwani bado timu hiyo ina safari ndefu.
“Safari kwanza ndiyo imeanza nawaomba hawa Precision Air waendelee kuidhamini timu hiyo kwani kwa kufanya hivyo, huo utakuwa ni msaada mkubwa kwa timu yetu hii ambayo inaonekana kama haina mwenyewe,”
Naye kwa upande wake anatoa wito kwa wadau mbalimbali wa michezo hapa nchini kujipanga kuisaidia timu hiyo ambayo itacheza na Ethiopia katika mzunguko mwingine kuanzia mwezi Aprili.
“Kwa kweli nikiwa kama mdau wa michezo nawapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kijituma na hatimaye kuliletea taifa letu sifa, jambo ambalo ni heshima kwa Watanzania wote” anasema
Kuhusu maandalizi ya timu hiyo kwa mzunguko wa pili, Dk.Ngozi anashauri kwamba timu hiyo inapaswa iingie kambini mapema na ipate michezo mbalimbali ya majaribio kabla ya kukwaana na wahabeshi hao.
“Mimi nadhani tusibweteke, tuiandae timu yetu vizuri, tujipange, tupange kuwa na michezo mbalimbali ya kimataifa ya majaribio ili tuweze kufanya vizuri,”
Anasema kwamba kwa kuwa timu zetu nyingine za taifa za soka, zimekuwa hazifanyi zizuri na hivyo kuwakataisha tamaa wadau mbalimbali wa soka, kwa sasa hatuna budi kuwekeza kwa kwenye timu hiyo ya wanawake ili angalu heshima yetu irudi.
“Serengeti Breweries ,benki ya NMB wanamwaga mamilioni ya fedha kila mwaka kwa timu ya taifa ya wanaume lakini pamoja na udhamini huo timu hiyo bado imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu, kwanini tusiwekeze kwenye timu ambayo inatutoa kimasomaso Watanzania?’ “ anahoji.
Anatoa wito kwa makampuni mbalimbali ya hapa nchini kuisaidia timu hiyo kwa upande wa maandalizi ya mzunguko unaofuata ili hatimaye timu hiyo iweze kufanya vizuri.
Mbali na Dk.Ngozi, wadau mbalimbali wa soka hapa nchini wanaishauri TFF kuweka program nzuri ya mazoezi ambayo itaiwezesha timu hiyo kujiandaa na kufanya vema katika mzungu wa pili.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Precision Air, Anet Nkini, anasema kwamba kampuni yake itaendelea kuiunga mkono sekta ya michezo kwa ujumla hapa nchini ili hatimaye timu zetu mbalimbali ziweze kuipeperusha vema bendera ya nchi yetu.
0 comments:
Post a Comment