Mtanange mkali wa kufa paka unataraji kupioga hii leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam baina ya timu mbili za Wacheza Filamu za Bongo na ile ya wanamuziki wa Bongo.
Mchezo huo maalum kwaajili ya kuwachangia fedha wahanga wa mafuriko jijini Dar es Salaam unataraji kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki akiongoza wasanii na wapenzi wa soka nchini kushuhudia mechi hiyo.
Mechi hiyo ni maalumu kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana. Akizungumza jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Compact Media inayoratibu mechi hiyo Elia Mjata alisema kuwa fedha zitakazopatikana katika mchezo huo zitapelekwa kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo.
Alisema kuwa kiingilio cha chini itakuwa ni shilingi 2,000 na kwa viti maalumu itakuwa Sh 30,000. Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, wasanii wa filamu juzi walitembelea Mabwepande kwa ajili ya kujua mahitaji ya waathirika hao.
Mjata alisema, wakati mkuu wa mkoa akiwaongoza wasanii wa filamu, Mkuu wa kanda maalamu ya kipolisi mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova atawaunga mkono wasanii wa muziki.
Alitaja baadhi ya wasanii wa dansi watakaoshiriki kuwa ni Chalz Baba, Ally Choki, Khalid Chokoraa, Kalala Junior, Nyoshi El Saadat na wengineo. Katika Bongo Movies aliwataja baadhi kuwa ni Steve Nyerere, Steven Kanumba na Richie Richie. Alisema kuwa pia wasanii wa muziki wa dansi watapata nafasi ya kuimba kwa pamoja.
0 comments:
Post a Comment