MASHABIKI wa mchezo wa mbio za magari mjini Arusha wamesherehekea miaka 50 ya Uhuru kwa kushuhudia madereva wakitoana jasho kwenye mashindano ya Uhuru Auto Cross.
Mahindano hayo yaliandaliwa na Kampuni ya mashindano ya magari ya Baba Dee Timu ya mjini hapa yalifanyika eneo la Meserani nje ya mji na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa.
Jumla ya magari 14 yalishiriki mashindano hayo yaliyovuta hisia za wapenzi wa mbio hizo kutokana na kuonyeshwa mbwembwe na umahiri wa madereva.
Dereva Sataji Hans akisaidiwa na Michael Ojare wakitumia gari aina ya Mitubishi walishika nafasi ya kwanza na kukabithiwa Sh. Milioni Moja, vikombe pamoja na cheti cha kushiriki mashindano hayo.
Washindi wengine waliokabidhiwa vyeti ni pamoja na Dereva aliyeshika nafasi ya pili Sh 700,000 na dereva aliyeshika nafasi ya tatu Sh. 500,000.
Akizungumza katika mashindano hayo mara baada ya kutoa zawadi kwa washindi Mbunge wa Monduli Lowassa aliwapongeza washiriki wa mbio hizo kwa kuonyesha umahiri mkubwa wa kuhimiri mikikimiki ya barabarani.
“Nimefurahi kuhudhuria mashindano yenu mmefanya vizuri naomba muendelee, nawapongeza washindi na ninategemea wale ambao hawakushinda basi mashindayo yajayo watakuwa washindi,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Endeleeni kushiriki mchezo huu ni kazi nzuri niwahakikishie kuwa mkinialika tena safari nyingine nitakuja,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Baba Dee Timu, David Kadawawa akizungumzia changamoto zinazoukabili mchezo huo wa magari nchini alisema, mpaka sasa wanakabiliwa ukosefu wa magari ya mashindano.
“Huu ni mchezo unaopendwa na watu wengi, lakini kwa hapa nchini hatuna kampuni maalumu za kuleta magari ya mchezo huu. Nadhani umefika wakati wa serikali iwekeze katika mchezo huu,” alisema Baba Dee na kuongeza:
“Lakini pia tunadhani kukipatikana kampuni au mtu kuingiza magari ya mashindano kwani madereva wengi wanapenda kushiriki mchezo huu lakini hawana magari maalumu,” alisema.
Hata hivyo Baba Dee alibainisha changamoto nyingine inayoukabili mchezo huo kuwa ni upatikanaji wa maeneo ya wazi ya kuendeshea magari ya mashindano.
“Mbali na maeneo ya wazi lakini pia, washiriki au madereva wengi wamekuwa wakiingia kushiriki bila kuwa na mafunzo na kujua kanuni za mchezo wa mbio za magari.
“Wengi wanaingia kwa kupewa maelekezo ya kawaida tu, hawana mafunzo hivyo kuwafanya wasiwe na vigezo vya kushiriki mashindano ya magari nje ya nchi,” alisema Baba Dee.
0 comments:
Post a Comment