Nafasi Ya Matangazo

December 16, 2011

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa International Conference on Great Lakes Region (ICGLR) wamekubaliana kuwa kila nchi wanachama itunge sheria za kupambana na ukatili wa kijinsia kama njia ya kuongeza amani na utulivu katika eneo hilo la Maziwa Makuu.
 
Rais Kikwete pia amesema kuwa mbali na kutunga sheria za namna hiyo, wakuu hao wa nchi wanachama za ICGLR wamekubaliana kuweka mifumo ya kuhakikisha kuwa sheria hizo zinafanya kazi kama njia ya kuondokana na tatizo la ukatili wa kijinsia katika eneo la nchi hizo.

Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Desemba 16 wakati alipotoa neno la shukurani wakati wa kipindi cha kufunga mkutano wa nne wa wakuu wa nchi hizo uliomalizika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, na kufungwa na Rais wa Uganda, Mheshimiwa Yoweri Museveni.

Tanzania ni nchi kiongozi katika eneo la Maziwa Makuu katika sheria, kanuni na taratibu za kupambana na ukatili wa kijinsia na baadhi ya makosa ya ukatili wa namna hiyo yanaadhibiwa kwa adhabu kali ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka 30 bila nafasi ya faini.

Akizungumza kwenye siku ya pili na ya mwisho ya mkutano huo wakati akitoa salamu za shukurani kwa wenyeji wa mkutano huo, Uganda, kwa niaba ya viongozi wenzake, Rais Kikwete ameuambia mkutano huo:

“Ni jambo la kutia moyo kuwa tumejadili kwa kina kabisa hali ya usalama na masuala ya maendeleo katika eneo letu. Tumejadili suala la ukatili wa kinjinsia na tumedhamiria kupambana na balaa hili. Azimio letu la kutokuvulimia kabisa balaa hili ni ujumbe wa kutosha wa matumaini kwa waathirika wa balaa hili na wale wanaoweza kunaswa katika janga hili,” Rais Kikwete amewaambia mamia ya wajumbe wa mkutano huo.
Mbali na maamuzi mengine, wakuu hao katika kikao chao cha leo wameamua kumteua Profesa Lumu Alphone Ntumba Luaba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa Katibu Mtendaji mpya wa ICGLR. Profesa Luaba anachukua nafasi ya Balozi Liberata Mulamula wa Tanzania ambaye amemaliza muda wake.
Wakati wa hotuba yake, Rais Kikwete amemwambia Profesa Luaba: “Tumemaliza mkutano wetu kwa furaha baada ya kumteua Profesa Lumu Alphone Ntumba Luaba kutoka DRC kuwa Katibu Mtendaji mpya wa ICGLR. Tunakupongeza. Tumekuteua kwa sababu Mawaziri wetu wametushawishi kuwa unafaa kwa kazi hii. Tafadhali thibisha ukweli hu kwa ubora wa kazi yako.”
Kwa Balozi Mulamula, Rais Kikwete amesema: “Kwa Balozi Mulamula, tunakushukuru sana kwa kazi yako nzuri uliyoifanyia Umoja wetu. Ulikuwa na kazi isiyokuwa ya kuonewa wivu ya kuanzisha sekretarieti ya umoja wetu tokea mwanzo kabisa. Umeifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa. Tutakukumbuka siku zote kwa mchango wako murua kwa umoja wetu.”

Balozi Mulamula ameongoza sekretarieti ya ICGLR kwa miaka mitano ya mwanzo. Muda wa uongozi wake ulimalizika mwaka jana, lakini katika mkutano maalum wa wakuu wa ICGLR uliofanyika mwaka jana Lusaka, Zambia, wakuu hao walimwomba balozi huyo kuendelea kuongoza Umoja huo kwa mwaka mmoja wa ziada wakati mrithi wake akitafutwa.

Mbali na Rais Kikwete, marais wengine wa nchi wanachama wa ICGLR waliohudhuria mkutano wa mwaka huu ni pamoja na Rais Yoweri Museveni, mwenyeji wa mkutano huo na mwenyekiti mpya wa ICGLR na Rais Michael Chilufya Satta wa Zambia ambaye amemaliza muda wake wa uenyekiti wake wa Umoja huo.

Marais wengine ni Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois.
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Desemba 16, 2011
KAMPALA
Posted by MROKI On Friday, December 16, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo