Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, (wa kwanza kushoto) akiwakabidhi vifaa vya ujenzi mabati 30 na mbao 50 , akina mama wawili wa Mtaa wa Kihonda Kazkazini karibu na Mizani,katika
Manispaa ya Morogoro, ambao uwezo wao ni mdogo baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa iliyonyesha juzi mjini hapa.
MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood ( CCM), ametoa msaada wa mabati 30 na mbao 50 kwa wakazi wawili wa Mtaa wa Kihonda Kaskazini , Manispaa ya Morogoro ,ambao uwezo wao ni mdogo wa kuweza kukarabati nyumba zao ambazo ziliezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua iliyotokea mwanzoni mwa wiki.
Upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa iliyonyesha alasiri ya Desemba 27, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro, ilisababisha baadhi ya wananchi wa Kata ya Kihonda , nyumba zao kuezuliwa na upepo huo na nyingine kujaa maji sambamba na kuharibu baadhi ya miundombinu ya barabara zilizimo ndani ya Kata hiyo.
Akikabidhi msaada wa vifaa hivyo kwa wakazi hao wawili , Mbunge huyo alisema , alipoarifiwa kuhusu kutokea kwa upepo na mvua kubwa zilizosababisha baadhi ya nyumba kadhaa kuezuliwa, alifika eneo hilo kujionea athari na kuoneshwa nyumba mbili zikiwa zimeezuliwa mapaa na wenyewe hawana uwezo wa kuzikarabati kwa haraka nyakati hizi za mvua.
“ Binafsi yangu nikiwa Mbunge niliguswa sana mara baada ya kufika eneo la tukio muda mfupi ,nikaoneshwa nyumba hizi mbili na kuona madhara makubwa ya paa kuezuliwa na wenyewe kukosa makazi” alisema Mbunge huyo na kuongeza.
“ ….sikuwaaidi kitu chochote , lakini kutokana na mvua hizi kuzidi kuendelea , nikaguswa na kuwahurumia wakiwemo watoto na baada ya wao kunieleza walivyopata shida kuzijenga nyumba zao , hivyo leo ( juzi Des 28) nimewaletea msaada wa mabati 30 na mbao 50 ili wawezekuziezeka tena na waendelee kuishi kwenye makazi yao” alisema Mbunge huyo.
Nao waathirika hao, Emmy Daniel na Mariam Mathayo, ambao nyumba zaoziliharibiwa vibaya kwa mapaa kuezeuliwa na upepo ulioambatana na mvuahizo, kwa nyakati tofauti walimshukuru Mbunge huyo kwa kuwajalikuwasaidia msaada wa vifaa vya ujenzi kwa wakati mara baada ya kupatwa na madhara hayo.
“ Tunamwombea kwa Mungu Mbunge wetu Abood , kwa kujitoa kutusaidia kwani kutoka ni moyo na si utajiri, ametukimbilia wakati wa shida na ametuwezesha, uwezo wetu ni mdogo , tusingeweza kuzikarabati kwa muda muafaka nyumba zetu” alisema Mariam Kwa upande wake, Emmy, alisema upepo huo ulioambatana na mvua kubwa iliyoanza majira aya saa 9:30 siku hiyo, iliezua paa la nyumba yake yenye vyumba vitatu, jiko na stoo , lakini watoto wake walisalimika.
“ Nilipigiwa simu nikiwa ndani ya Daladala ni kirejea nyumbani, kuwa nyumba umeezuliwa na upepo, na watoto wamehifadhiwa na majirani ,sikuwa na namna , lakini nina mshukuru mbunge kwa msaada wake huu kwetu” alisema Mkazi huyo.
Naye Balozi wa Mtaa huo, Ahmed Saadi, alisema tathimini waliyoifanya baada ya upepo na mvua hizo kukoma , walibaini nyumba 11 likiwemo jengo la shule ya Seminari iliyopo eneo hilo la Kihonda sehemu ya paa lake kuezuliwa sambamba na nyumba hizo kwa viwango tofauti.
Alisema, madhara hayo yamechangiwa na eneo hilo kutokuwa na miti yakuzuia upepo , pamoja na ukosefu wa mifereji katika barabara za mitaa hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni makazi mapya.
Hata hivyo aliwataka baadhi ya wananchi waliojenga kwenye mikondo ya maji na mabondeni wachukue tahadhari kwa vile mvua za mwaka huu zinaonesha zitakuwa na madhara makubwa kwa watu waliojenga maeneo hayo.
Source: John Nditi wa Habarileo
0 comments:
Post a Comment