Nafasi Ya Matangazo

October 19, 2011

Mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kwegyir akitokwa machozi baada ya kumuona kijana Robert Tangawizi (14) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) alivyojeruhiwa mkono wa kushoto na kisha kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kulia, wakati alipomtembelea hospitalini Geita mkoani Mwanza.
 
WATU watano wakiwemo baba mzazi na mama wa kambo wa kijana mlemavu wa ngozi, Adam Robert, wamekamatwa na Polisi wilayani Geita Mkoa wa Mwanza, kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata mapanga na kumnyofoa vidole vitatu kijana huyo, mkazi wa Kijiji cha Nyaruguguna.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, lakini alikataa kuwataja majina.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, zimeeleza kuwa miongoni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na mganga maarufu wa jadi, Rumanyika Yesu (49).

Wengine kwa mujibu wa taarifa hizo ni pamoja na baba mzazi wa Adam, Robert Tangawizi (36), mama wa kambo wa majeruhi huyo ambaye amekuwa akimlea kwa siku nyingi, Agnes Majala (29).

Pia baba mkubwa wa Adam, Andrew Tangawizi (52) na mkazi wa kijiji hicho, Machibya Alphonce (30). Taarifa hizo zimeeleza kuwa baba mzazi amekamatwa kutokana na maelezo ya mtoto na mazingira ya tukio hilo.

Adam anadaiwa kueleza kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa ambaye ametoroka na anatafutwa na Polisi, alitaka kufanya kitendo hicho machungani, lakini mtoto huyo alimzidi ujanja.

Katika maelezo hayo, Adam alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alimdanganyia kofia, lakini alikataa kabla ya kumtaka kuwapeleka ng’ombe kwenye nyasi nyingi ambapo kulikuwa na kichaka, lakini pia alikataa.

“Siku hiyo hiyo jioni mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwao na mtoto na kisha akakaribishwa na baba mzazi na kuketi naye mahali walipokuwa wakiota moto (Kikome).

“Ghafla mtoto alianza kumweleza baba yake kuwa mtu huyo alikuwa akimfuatafuata machungani na baba yake alimvuta pembeni na kumsikiliza kisha wakarudi na kuketi pamoja kwenye Kikome,” chanzo chetu kilinukuu maelezo yaliyoandikwa Polisi.

Katika maelezo hayo, mtoto huyo alidai kuwa baada ya kuketi, chakula kililetwa, lakini kabla ya kuanza kula, mvua ilianza kunyesha na ndipo baba alipochukua ugali na kumtaka mtoto kubeba mboga kwenda ndani.

“Lakini ghafla mtuhumiwa huyo alimgeukia mtoto huyo na kumuangusha chini kisha kuanza kumkata mkono kabla ya kumng’ata sehemu za siri na kumuachia.

“Hawa wazazi wote tunaowashikilia, inavyoonekana wanalijua jambo hili kwa sababu kwa mfano huyu baba mkubwa wa mtoto siku hiyo aliamua kumfuata kaka yake na majeruhi, ambaye pia ni albino kwa ajili ya kwenda kulala nyumbani kwake ambako ni umbali wa kilometa moja na nusu.

“Na huyu mama wa kambo pamoja na kitendo kufanyika nje ya nyumba alimokuwa ndani, wakati mtoto akipiga kelele hakuweza hata kutoka ndani,” kiliongeza chanzo chetu.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Al- Shaymaa Kwegyir (CCM) ambaye pia ni mlemavu wa ngozi jana alijikuta akiangua kilio hadharani katika Hospitali ya Wilaya ya Geita alikolazwa majeruhi huyo, mara baada ya kuingia wodini na kumuona mtoto huyo ambaye amejeruhiwa.

Al-Shaymaa aliwasili mjini Geita saa 6 mchana na kwenda moja kwa moja katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kupata maelezo ya awali.

Baada tu ya kuingia wodi namba 8 ya hospitali hiyo alikolazwa mtoto huyo na kutazama majeraha yake, alijikuta akiangua kilio huku akiwa amemshika majeruhi huyo kichwani.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, alisema kitendo alichofanyiwa mlemavu huyo ni cha kinyama, ambacho hapaswi kufanyiwa binadamu na kuhoji waliotenda unyama huo ni binadamu au wanyama?

“Hivi Watanzania tunakwenda wapi?...unyama wa namna hii umefanywa na binadamu kama mimi ama mnyama?... kama ni hivi ni bora kuishi na mnyama, lakini siyo binadamu,” alisema huku akifuta machozi.

“Jamani mimi hii ni mara yangu ya pili kuja Geita, lakini nakuja Geita kwa matatizo tu, nilikuja hapa kuwachukua wale albino waliokatwa miguu kwenda nao Dar es Salaam, lakini leo tena nimekuja kwenye tatizo kama hilo, jamani tumuogope Mungu hawa ni binadamu kama sisi,”
alisema.

Alisema anafanya utaratibu wa kumhamishia mtoto huyo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa kuwa mtoto huyo pamoja na kaka yake waliachishwa masomo tangu mwaka 2008, yeye kwa kushirikiana na Shirika la Under The Same Sun watawasomesha watoto hao.

Mlemavu huyo alijeruhiwa usiku wa kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita saa 2 katika Kijiji cha Nyaruguguna, na kukatwa mkono wa kushoto kabla ya kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kulia.

Chanzo:Habarileo
Posted by MROKI On Wednesday, October 19, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo