Nafasi Ya Matangazo

May 29, 2011

Na Mwandishi Wetu

MPIGAPICHA Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, ambaye pia ni Mmiliki wa Blogu ya Kamanda wa Matukio, Richard  Mwaikenda ameporwa begi lenye kamera na kompyuta na vibaka waendesha pikipiki.

Vibaka hao waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki, walimpora begi hilo lililokuwa kiti cha mbele cha gari lake alilokuwa akiendesha, likiwa karibu na makutano ya barabara za Kitunda na Nyerere, eneo la Banana, Ukonga, Dar es Salaam Jumamosi wiki iliyopita.

Aliyechukua begi kwenye gari ni kibaka aliyepakizwa nyuma na pikipiki hiyo kuondoka kwa kasi kuelekea
Ukonga na kumwia vigumu mpiga picha huyo kuachia usukani kuwafukuza kwani magari yalikuwa yameanza
kutembea.

Alitaja vitu vingine vilivyokuwemo kwenye begi hilo kuwa ni, Modemu ya Vodacom, kifaa cha kutolea picha kutoka kamera ya digito kwenda katika kompyuta (Cardreader), Flash, vitambulisho vya kazi na nyaraka muhimu.

Akisimulia tukio hilo, Mwaikenda alisema , inaelekea vibaka hao walimfuatilia kutoka Kitunda ambapo
alisimamisha gari lake na kuchukua kamera kwenye begi na kupiga picha mashimo makubwa barabarani karibu na Kituo Kidogo cha Polisi cha Kitunda.

Mwaikenda alikuwa anatokea nyumbani kwake, Kivule kwenda Pugu Kanisani kuripoti tukio la Ibada ya misa ya shukrani kwa Hayati Papa John Paul wa Pili kutangazwa Mwenye Heri.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mwaikenda alisema alitarajia kutoa taarifa Polisi juu ya wizi huo wa kutumia pikipiki ambao umekithiri katika miji mbalimbali.

Hii ni mara ya pili kwa Mpigapicha huyo kuibiwa Camera yake ambapo awali aliibiwa wakati akirejea nyumbani akitoka kazini.

 Aidha Camera iliyoporwa juzi ni zawadi aliyoipata kutoka MCT baada ya kuibuka Mpiga picha bora katika Tuzo za Wanahabari za Mwaka 2009/2010.
Posted by MROKI On Sunday, May 29, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo