Nafasi Ya Matangazo

December 07, 2010

 Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria ktk mkutano wa hadhara uliondaliwa na CCM Wilaya ya Newala kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua Mhe. Mkuchika (hayupo pichani) kuwa Mbunge wao katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo mjini Newala.
Wawakilishi wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Newala wakijiandaa kumkabidhi zawadi ya ua mbunge wa Newala, Mhe. George Huruma Mkuchika Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu - TAMISEMI katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wanachi wa Newala kwa kumchagua kuwa mbunge wao.

Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Newala kimempongeza Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais, na pia kimemshukuru kwa kumteua Mbunge wa Jimbo la Newala kuwa Waziri.

Hayo yalikuwa ni moja ya maazimio ya kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Newala kilichofanyika leo katika ukumbi wa Umoja mjini Newala. Aidha Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Newala kimemwahidi Mhe. Jakaya Kikwete ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chama hicho kwamba wataendelea kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi ili kiindelee kuwa Chama tawala.

Halmashauri Kuu ya CCM Newala pia imewaagiza madiwani waliochaguliwa kutunga sheria ndogo itakayosimamia utoaji wa michango ya ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita kwa kila Tarafa na kuimarisha Sekondari za Kata zilizopo sasa.

Azimio linginge lililopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Wilayani Newala ni uanzishwaji wa Benki ya Wananchi wa Newala katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi yaani mwaka 2010-2015. Aidha wameliagiza Baraza la Madiwani kusimamia utekelezaji wake mara watakapo apishwa.

 Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Newala, Mhe. George Huruma Mkuchika ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), amewashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya kwa kusimamia na kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010, “Nawashukuru sana kwa kazi nzuri mriyofanya wakati wakampeni, maana mlijitoa kwa moyo na mkaweka kando tofauti za kura za maoni na ndio maana tumeshinda vizuri, asateni sana, naomba shukurani hizi mzifikishe kwa viongozi wa Matawi, Mabalozi na wanchama wote”, alisema Mh. Mkuchika.

Mheshimiwa Mkuchika ameahidi kushirikiana na wananchi wote wa Newala katika kuhamasisha maendeleo ya Wilaya hiyo, “Naomba ushirikiano wenu katika kuhamasisha maendeleo ya Newala, mimi ni mbunge wa watu wote, na hapa naahidi kwamba ili tufikie azma ya maendeleo ya kweli , nitawashirikisha mpaka viongozi wa vyama vingine vya siasa katika mikutano ya kuhamasisha maendeleo,”

Mapema asubuhi kabla ya kuhutubia Kikao cha Halmashauri kuu ya CCM ya Wilaya ya Newala, Mheshimiwa Mkuchika amekutana na watendaji wa serikali katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jingo la Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Mkuchaika amewataka watendaji wa Serikali kuwajibika na kufanya kazi kwa mjibu wa sheria , taratibu na kanuni zilizopo za serikali kuu na serikali za Mitaa.

Aidha amewaomba wampe ushirikiano mzuri katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchguzi kwa maslahi ya maendeleo ya wana Newala, na amewataka wakuu wa idara wote kusoma na kuielewa vizuri ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ili waweze kusimamia vizuri utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mkuchika yupo jimboni Newala kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kwa mara nyingine tena kuwa Mbunge wao. Kesho ataendelea kuhutubia mikutano ya hadhara ya kuwashukuru wananchi wa tarafa za Chilangala, Kitangali na Mkunya.
Posted by MROKI On Tuesday, December 07, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo