Serikali imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa juhudi zake za kuboresha uendeshaji wa bandari nchini, hatua inayoongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma huku ikichangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza mkoani Pwani baada ya kutembelea Bandari ya Nyamisati, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema maboresho yaliyofanyika yameifanya sekta ya bandari kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza kasi ya kuhudumia mizigo, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini, na kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara na kampuni.
“Hatua hizi zimeongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” amesema Naibu Waziri Kihenzile.
Aidha, ameitaka TPA kuhakikisha miradi ya ujenzi wa bandari za Bagamoyo, Kisiju na Nyamisati inawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo huduma za kijamii na uboreshaji wa miundombinu katika maeneo yanayozunguka bandari.
Kuhusu usafiri salama majini, Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaendelea na tafiti za kitaalamu ili kubaini mahitaji halisi na kuimarisha huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema maboresho yanayotarajiwa ni pamoja na uboreshaji wa jengo la abiria ili kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja, pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mingine ya bandari.









0 comments:
Post a Comment