Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya Shilingi Bilioni 42 kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya Maji Wilayani Monduli Mkoani Arusha na kuridhia kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu- Selela huku kipande cha Selela- Engaruka usanifu ukikamilika na kuanza kwa mchakato wa kupatikana kwa Mkandarasi.
Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Monduli leo Alhamisi Januari 08, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amesema Mkandarasi wa kutekeleza ujenzi wa Barabara ya Mto wa Mbu- Selela na Monduli Chini kwenda Monduli juu ikiwa na urefu wa Kilomita 11 tayari wamepatikana.
"Kipande cha Mto wa Mbu- Selela (Km23) Mkandarasi amepatikana na ataoneshwa eneo la kazi (site) hivi karibuni na kipande cha pili ni Selela- Engaruka (Km27) na hiki usanifu umekamilika na mchakato wa kumpata Mkandarasi unaendelea. Barabara hii ni muhimu kwa mradi wa Kimkakati wa Magadisoda, utalii wa Ziwa Natroni pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii." Amesema Mhe. Makalla.
Mhe. Makalla pia ametangaza kuanza kwa taratibu za kulipwa kwa fidia kwa wananchi wa Meserani Wilayani Monduli, ambao watapisha ujenzi wa Mzani wa kisasa utakaohamishwa kutoka Makuyuni kwenda katika eneo hilo na itakayojengwa kwa pande zote mbili za barabara, lengo likiwa ni kupunguza foleni kwa magari katika Mzani wa sasa wa Makuyuni ambao upo kwa upande mmoja pekee.


.jpeg)






0 comments:
Post a Comment