Nafasi Ya Matangazo

November 16, 2010

KAMPUNI ya Simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imepata msaada wa dola za Kimarekani

milioni 4.8 kutoka kwa mfuko wa Bill & Melinda Gates Foundation ili kuiwezesha kampuni hiyo

kupanua wigo wa utoaji huduma kupitia huduma yake ya kifedha ya Vodafone M-PESA.



Akizungumza kuhusiana na msaada huo walioupata Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom

Tanzania, Dietlof Mare, alisema utasaidia kuboresha hali ya maisha ya Watanzania kama

kampuni hiyo inavyoamini kuwa huduma ya Vodafone M-Pesa imechangia kukua kwa sekta ya

kifedha nchini.



Aidha Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa msaada huo ambao una thamani ya fedha za

Kitanzania bilioni 7.2/- utasaidia upatikanaji wa huduma za M-Pesa na wateja wataweza

kupokea fedha kutoka kwa mawakala katika maeneo yao.



“Huduma ya Vodafone M-Pesa inayotolewa na Vodacom Tanzania imeongeza uwajibikaji na

upatikanaji wa huduma za kifedha hususani hadi katika maeneo yote ya nchi ambayo hayafikiki

kiurahisi,” alisema Mare.



“Tanzania ni nchi inayaokadiriwa kuwa na watu takribani milioni 40, na kwamba ni wachache tu

ndio wanaofikiwa na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi mbalimbali. Hadi sasa takwimu

zinaonesha kwamba miongoni mwao ni watu milioni mbili tu wenye akaunti benki, wakati zaidi

ya milioni 18 wanatumia huduma hiyo kupitia simu za mkononi,” aliongeza.



Utafiti uliofanyika hivi karibuni nchini Kenya umeonesha kwamba watu wengi wanaona huduma

za M-Pesa ni salama na ni rahisi katika uhifadhiji fedha, kutuma na hata kupokea kwa marafiki,

wanafamilia na wadau katika biashara.



Kwa mujibu wa Mare, ni kwamba kampuni hiyo ndiyo pekee iliyopatiwa msaada huo kutokana

na misingi yake iliyojiwekea katika huduma hiyo ya kusafirisha fedha kwa njia ya simu za

mkononi nchini na uwekezaji mkubwa iliyoufanya katika teknolojia hiyo.



Hadi sasa inakadiriwa kwamba nchini kuna zaidi ya watu milioni 5.3 ambao tayari

wamekwishajisajili katika kutumia huduma hii ya Vodafone M-PESA.


 
Vilevile imebainika kwamba katika maeneo ambayo huduma za kifedha zilikuwa hazifiki, benki

za kijamii zimeshindwa kujiendesha baada ya huduma hiyo kufika jambo lililochangiwa na

uhamasishaji, usalama katika utoaji huduma, upatikanaji wa huduma bora.



Kupitia msaada huo wa Bill & Melinda Gates Foundation kwa huduma za kifedha kwa miradi ya

watu masikini , Vodacom itapanua wigo wa huduma hii ili kuweza kufika maeneo mengi zaidi ya

jamii isiyofikiwa na taasisi za kifedha.



Msaada ulitangazwa kutolewa rasmi kutolewa na mfuko huo wa Melinda French Gates mjini

Washington Novemba 16 mwaka huu ikiwa ni miongoni mwa jumla ya dola za Kimarekani

milioni 500 zilizotolewa ili kuinua upatikanaji wa huduma za kifedha na kuzijengea nchi maskini

uwezo wa kuboresha huduma salama za kifedha.



Aidha mfuko huo umeahidi kutoa kwa vipindi sita jumla ya dola za Kimarekani milioni 40 kutoka

kwenye mfuko huo wa huduma za kifedha kwa miradi ya watu masikini ili kusaidia miradi na

wadau wake kutoa huduma bora, upatikanaji wa akaunti za akiba na huduma zingine za kifedha

zinazofikika hadi kwenye milango ya ya jamii zilizo kwenye nchi zinazoendelea.



“Uwekaji fedha kwenye akaunti hakumsaidii mtu kujiepusha na kufikwa na matatizo ya

kitabibu ama kupata mavuno mabaya,” alisema Gates wakati wa hafla ya mfuko huo.


“Lakini unaiwezesha jamii kujijengea rasilimali zitakazoiwezesha kufanya kilicho bora zaidi

kwao na hata kwa watoto wao. Pia unawaongezea kuanzisha biashara zao, zitakazowafanya

kufika mbele kwa kujiamini. Akiba inasaidia familia kukua kimaendeleo kutoka hatua moja hadi

nyingine na kuwa zenye afya na zenye furaha.”

Posted by MROKI On Tuesday, November 16, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo