Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Tume ya Madini imewaalika wawekezaji, wafanyabiashara, vijana, wanawake na wananchi kwa ujumla kutembelea banda lake katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yanayoendelea kufanyika Fumba, Zanzibar, ili kujifunza na kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Kupitia maonesho hayo, Tume inaonesha fursa katika utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini, biashara ya madini pamoja na utoaji wa bidhaa na huduma kwa shughuli za migodini.
Aidha, Tume inaeleza mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema kuwa sekta ya madini inatoa fursa jumuishi kwa makundi yote, ikiwemo wachimbaji wadogo na wajasiriamali, na kuwahimiza wananchi kuomba Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PML), kushiriki katika shughuli za uongezaji thamani wa madini pamoja na kutumia masoko rasmi ya madini na vituo vya ununuzi wa madini.
Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yataendelea hadi Januari 16, 2026, na wananchi wote wanakaribishwa kutembelea Banda la Tume ya Madini kwa ajili ya kupata elimu, ushauri na kugundua fursa za uwekezaji zinazoweza kubadilisha maisha katika sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini Tanzania.









0 comments:
Post a Comment