Nafasi Ya Matangazo

May 13, 2012

Nimesikitishwa na kushangazwa na taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari hivi leo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.

Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera. Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi. Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.

Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa. Lakini vilevile, ningetegemea kwamba, kama ameamua kusambaza taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki Kuu.

Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni, kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.

Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo. Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.

Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.

Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe. Hili limenishangaza kwasababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni. Huu ni utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.

Pili, ningetegemea pia Mhe. Zitto awe anafahamu kwamba kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board). Huko nyuma, Kamati hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika Benki Kuu vipunguzwe. Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati hii inayopitisha taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili. Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu. Mara ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari, ambayo

imekwishasambazwa.

Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka. Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo. Mimi ndicho nilichofanya, na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja kama alivyodai Mhe ZITTO. 

Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia tarehe 11 May 2012). Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.

Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.

Imetolewa na:
Mwigulu Lameck Nchemba (MB)
Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa
Dodoma
13 Mei 2012

Posted by MROKI On Sunday, May 13, 2012 1 comment

1 comment:

  1. AnonymousMay 13, 2012

    Nani anasema ukweli hapa?Hebu ondokeni mnatusumbua tu sisi walalahoi huku kijijini ambako kama hela zipo hazina au hazipo maisha magumu palepale.

    ReplyDelete

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo