Kaimu
Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania
(ATCL) Paul Chizi akiongea na waandishi wa habari mara bada ya kuwasili
kwa ndege mpya aina ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na shirika hilo
yenye uwezo wa kubeba abiria 108.
Wafanyakazi
wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakikata keki kusherekea ujio wa
ndege ndege mpya aina ya Boeing 737-500. Wapili kushoto ni Kaimu
Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL)
Paul Chizi
Wafanyakazi
wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakishuka katika ndege mpya aina
ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na shirika hilo yenye uwezo wa kubeba
abiria 108. Ndege hiyo itaanza kuruka bada ya wiki moja.
Mmoja
wa wafanyakazi wa ATCL akiwaamebeba ujumbe wa kumkaribisha Waziri
Harisson Mwakyembe baada ya uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete
hivi karibuni.
Wahudumu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakipozi mbele ya kamera ya blogu hii.
========= ===== ===
NDEGE mpya aina ya Boeing 737-500 iliyokodishwa na Shirika la ndege la AIR Tanzania (ATCL) imewasili nchini wikiendi hii na itaanza safari za Dar-Mwanza-Kilimanjaro kabla ya kuanza safari za kimataifa, Kaimu Mkurugenzi na Mwenyekiti Mtendaji wa ATCL Paul Chizi amesema.
Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 108 iliyokodishwa toka kwa kampuni ya Aero Vista Dubai, Chizi alisema kuwa ATCL itaanza safari zake katika kipindi cha wiki moja kuanzia sasa na kuonyesha uwezekano wa kuiunganisha Dar es Salaam na Dubai katika safari zake katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
“Watanzania watarajie huduma bora waliyoikosa kwa kipindi kirefu sasa. Tutarudisha safari zetu katika kipindi cha wiki moja. Tunaitaji watuunge mkono kama ilivyokawaida yao katika siku za nyuma.
“Huduma zetu ni za uhakika na ni kwa ajili ya wateja wetu. Muda ni kigezo chetu kikubwa katika kazi na sasa tunatarajia kutoa huduma kwa wakati lakini pia huduma zenye unafuu kwa wateja,” alisema.
Chizi alisema kuwa kampuni inatarajia kuungana kibiashara na makampuni ya kimataifa ya ndege katika lengo la kutanua safari zake lakini alisisitiza kuwa hali hiyo itakuwa na faida na matunda pande zote mbili.
“Kupitia muungano huo wa kibiashara, tutahakikisha kuwa kila mmoja anafaidika. Ambapo katika muungano huo kampuni inapokosa faida, daima muungano huo wa kibiashara hauwezi kudumu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ndege nyingine ya kampuni hiyo aina ya Dash 8 ambayo inafanyiwa matengenezo Terminal 1 nayo itakuwa tayari katika kipindi cha wiki sita zizajo na itasaidia kuboresha utoaji huduma zaidi wa kampuni hiyo.
Ndege mpya ya ATCL Boeing 737-500 imeshafanyiwa uchunguzi na timu ya wataalam kutoka katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) jijini Cairo nchini Misri na tayari hati ya kibali cha ufanyaji kazi wa ndege hiyo nchini kimeshatolewa.
Ndege hiyo iliyonakshiwa na rangi za shirika la ndege la ATCL inachukua abiria wapatao 12 katika daraja la kwanza (business class) pamoja na abiria 96 katika daraja la kawaida (economy class)
ATCL hivi karibuni ilizindua tovuti katika lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kukuza ubora katika utendaji kazi wa shirika hilo la ndege la kitaifa.
Tovuti hiyo inawawezesha wateja kupata huduma za ukataji tiketi bila ya kufika katika ofisi za ATCL au kupitia mawakala na kuwasaidia wateja kutoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment