Kambi hiyo maalumu iliyofanyika kwa siku tatu imefanyika katika viwanja vya Mafia Boxing Sports Promotion vilivyopo Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo mabondia hao wamepimwa vipimo vikubwa vya kuchunguza moyo pamoja na vipimo vya awali vilivyowawezesha kujua namba zao za afya.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari wa magonjwa ya ndani waTaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Nelson Marwa alisema kambi hiyo ilikuwa na malengo ya kuwasaidia mabondia nchini kufahamu hali zao za afya na kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao wanapofanya mazoezi ama wanapokuwa katika mapambano ya ngumi.
“Mabondia tuliowafanyia uchunguzi wa afya wengi wao tumewakuta na hali nzuri kiafya jambo linaloridhisha, ni vyema baada ya leo wakaendelea kufanya uchunguzi wa afya zao kila wanapopata nafasi”, alisema Dkt. Marwa.
Dkt. Marwa alisema uchunguzi wa afya ni muhimu kwa mabondia kwa sababu kufanya mazoezi mara kwa mara na kujihisi mwenye nguvu hakumaanishi kuwa mtu hana tatizo la kiafya hivyo ni vyema wanamichezo wakapima afya zao hata pale wanapokuwa hawana dalili za ugonjwa.
“Wito wangu kwa mabondia wengine ambao bado hawajafanya uchunguzi wa moyo wajitokeze kupima afya zao ili waweze kujua hali zao na kuchukua hatua mapema ili kupunguza hatari ya vifo vya ghafla hasa wanapokuwa michezoni”, alisema Dkt. Marwa.
Kwa upande wake bondia wa ngumi za kulipwa nchini Nickson Jastin alisema changamoto za kipato na hofu ya kugundulika kuwa na ugonjwa ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwafanya baadhi ya wanamichezo kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
“Ni muhimu mtu akapima afya yake mara kwa mara ingawa wakati mwingine kipato kinaweza kuwa changamoto na wengine wanaogopa kupima kwa kuhofia watakachokikuta lakini unapofahamu hali yako ya afya unakuwa na uhakika zaidi wa kutekeleza majukumu yako”, alisema Jastin.
Naye bondia wa ngumi za kulipwa nchini Paul Sangu alisema amefurahishwa na huduma alizopata katika kambi hiyo akieleza kuwa baadhi ya kambi za mazoezi ya ngumi zimekuwa hazina utaratibu wa kuchunguzi afya.
“Katika gym nyingi hatuna utaratibu wa kupima afya kama ilivyofanyika hapa kwa hiyo ninawashauri mabondia wenzangu wakipata taarifa za huduma kama hizi wajitokeze kupima afya zao na kufanya vipimo vinavyohitajika kwa sababu afya ni muhimu”, alisema Sangu.
Kambi hiyo ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo karibu na wanamichezo na kuwahamasisha kutambua umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara.



.jpeg)



0 comments:
Post a Comment