Nafasi Ya Matangazo

October 20, 2026




Na. OWM (KAM), Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amezihamasisha Taasisi za Dini nchini kuwa daraja la amani kwa kushirikiana na Serikali ili kuimarisha mahusiano mema, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Sangu ameyasema hayo leo, Oktoba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada ya kuwekwa wakfu Askofu John Jumanne Wambura wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini, iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Aidha, amesema Falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayohusu Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Mpya inapaswa kuendelezwa kama sehemu ya utamaduni wa Taifa, huku akizitaka taasisi za dini kuendelea kuhimiza upendo, kuheshimiana, mazungumzo na utatuzi wa tofauti kwa amani ili kuimarisha umoja wa Watanzania.

Vilevile, Waziri Sangu amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika kuimarisha maadili, kutoa huduma za kijamii, elimu na afya, pamoja na kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu. Pia, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hizo katika kuimarisha mahusiano mema na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare, ameishukuru Serikali kwa kushiriki katika ibada hiyo, akieleza kuwa Kanisa litaendelea kuliombea Taifa, kuenzi upendo, kulinda amani na kuwa wajumbe wa amani. Aidha, ameahidi kuendeleza falsafa ya 4R katika Kanisa na kuhimiza uzalendo unaodhihirishwa kwa matendo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameahidi ushirikiano wa Serikali ya Mkoa na taasisi za dini, akieleza kuwa mafanikio ya huduma za Kanisa yana mchango katika ustawi wa jamii na maendeleo ya Mkoa, hususan kupitia maombi, malezi na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Katika ibada hiyo, Waziri Sangu amempongeza Askofu Wambura kwa kuaminiwa kuongoza Dayosisi ya Kaskazini, inayohusisha mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha, huku akimtaka kutekeleza majukumu yake kwa hekima, unyenyekevu na upendo. Amewahimiza Watanzania kuendelea kulinda amani na kujenga madaraja ya maridhiano kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.

Posted by MROKI On Tuesday, October 20, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo