Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema mradi wa Kongani ya Viwanda unaotekelezwa na mwekezaji Hongwang Tanzania Holdings wilayani Songea, mkoani Ruvuma, unatarajiwa kutoa ajira 5,000 kwa Watanzania.
Amesema hayo Oktoba 23, 2026, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, katika eneo la mradi huo unaohusisha uzalishaji wa megawati 2,000 za umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo makaa ya mawe, pamoja na viwanda vya aluminium na chuma.
Brigedia Jenerali Ahmed amesema mradi huo unagharimu dola za Marekani bilioni 3, sawa na takribani Sh trilioni 7.8, na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi mkoani Ruvuma kupitia fursa za ajira, uwekezaji na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme nchini.
Ameeleza kuwa sehemu ndogo ya umeme utakaozalishwa itatumika katika shughuli za viwanda vilivyopo ndani ya kongani hiyo, huku sehemu nyingine ikiuzwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuingizwa katika gridi ya taifa. Aidha, mwekezaji ameanza ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kwenda kituo cha kupokea umeme kilichopo Songea mjini.
Ameongeza kiwa mradi huo ni wa kimkakati kwa Ruvuma na utasaidia kupanua fursa za ajira na uwekezaji. Ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira yanayovutia wawekezaji na kuwataka wananchi wa mkoa huo kuwa walinzi wa miradi ya kimkakati, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuhakikisha usalama wa miradi na rasilimali zinazotumika.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Hongwang Tanzania Holdings amesema umeme utazalishwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo makaa ya mawe, huku kampuni ikiahidi kuzingatia miongozo ya mazingira na viwango vya kimataifa katika utekelezaji wa mradi huo.









0 comments:
Post a Comment