Nafasi Ya Matangazo

October 22, 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akizungumza wakati akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, lililofanyika Jijini Dar es Salaam, Oktoba 22, 2026.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha soko la kaboni barani Afrika, huku Serikali ikiimarisha mifumo ya usimamizi, uwazi na uwekezaji ili kuhakikisha biashara hiyo inachangia ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
 
Mhe. Masauni ameyasema hayo, Oktoba 22, 2026, wakati akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, lililofanyika Jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu isemayo “Siku Moja. Soko Moja. Maono ya Pamoja.”
 
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inakuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya jamii, kuvutia uwekezaji, kuhifadhi misitu na kuendeleza matumizi ya nishati safi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
 
“Tanzania imeamua kuwa kitovu cha soko la kaboni lenye uadilifu barani Afrika, soko ambalo kila tani ya kaboni inayothibitishwa inatafsirika kuwa ajira kwa vijana wetu, mapato kwa vijiji vyetu, misitu iliyohifadhiwa, nishati safi majumbani mwetu na mtaji wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Mhe. Masauni.
 
Amesisitiza kuwa mafanikio ya soko la kaboni hayatategemea wingi wa miradi pekee, bali ubora wa matokeo, uhalali wa kisheria, uwekezaji unaotekelezwa na manufaa halisi yanayowafikia wananchi.
 
Ameongeza kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ajenda ya nishati safi ya kupikia ni mojawapo ya maeneo yenye fursa kubwa ya biashara ya kaboni, kutokana na uwezo wake wa kufikia mamilioni ya kaya na kuchangia kupunguza gesijoto.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba ameongeza kuwa kituo hicho kina jukumu muhimu la kusaidia maendeleo ya soko la kaboni nchini kwa kuzingatia utaalamu wa kisayansi, mbinu sahihi za kitaalamu, uwazi wa taarifa na mifumo ya ufuatiliaji na uthibitishaji.
 
Amesema lengo ni kujenga soko ambalo miradi yake inatambuliwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaofaa, inafanyika kwa uwazi na manufaa yanayopatikana yanachangia maendeleo endelevu ya Tanzania.
 
Ameongeza kuwa utekelezaji wa azma hiyo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, waendelezaji wa miradi ya kaboni, wawekezaji, taasisi za fedha, jamii za wenyeji, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo.
 
Ameongeza kuwa mifumo ya kitaasisi inayohusu tathmini ya miradi, usajili wa miradi, ubadilishanaji wa taarifa na ulinzi wa haki na maslahi ya wadau ni muhimu katika kujenga imani ya soko.
 
Awali Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alisema jamii zinazohusika na usimamizi wa misitu, ardhioevu, mikoko na maeneo mengine yenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi kaboni zinapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kubuni na kutekeleza miradi pamoja na kupanga namna ya kugawana manufaa.

Aidha, wanawake, vijana, wajasiriamali wa ndani na waendelezaji wa miradi midogo wanapaswa kupata nafasi katika uchumi unaochochewa na soko la kaboni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akisalimiana na Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Bw. Sondre Bjotveit mara baada ya kuwasili Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam kwa ajili ya akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, lililofanyika, Oktoba 22, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akiwasili Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam kwa ajili ya akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, lililofanyika, Oktoba 22, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akiwasili Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam kwa ajili ya akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, lililofanyika, Oktoba 22, 2026.
Posted by MROKI On Thursday, October 22, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo