Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Juma Zuberi Homera amesema zoezi la uchimbaji
wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara limekamilika kwa
mafanikio makubwa, ambapo imegunduliwa gesi
asilia inayotarajiwa kuongeza kiasi cha nishati hiyo kutoka futi za ujazo trilioni 57.54 zilizopo sasa.
Amesema Serikali inatarajia
kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika Kijiji
cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa kutokana
na shughuli hizo za uchimbaji.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo, Oktoba 18, 2026, katika Ofisi
Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Mhe. Homera amesema visima hivyo, viwili vya uendelezaji na
kimoja cha utafiti, vimechimbwa
kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na mwekezaji,
kampuni ya M&P.
Amesema ugunduzi huo unazidi
kuiwezesha Serikali kuwa na nishati ya gesi
asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji
katika sekta hiyo.
Mhe. Homera ameongeza kuwa
Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli
za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo
Songo Magharibi, Mnazi Bay
Kaskazini na Ntorya.
Ameeleza kuwa shughuli za
uchukuaji wa data za mitetemo zinaendelea
katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na zinatarajiwa kukamilika Desemba 2026, huku
maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha uzalishaji
na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea
katika Kitalu cha Ntorya.
Kuhusu maendeleo ya Kitalu cha
Ntorya, Mhe. Homera amesema ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya hadi Madimba umefikia asilimia 70 na
unatarajiwa kukamilika Desemba 2026,
huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa
siku.
Ameeleza kuwa TPDC inaendelea
kushirikiana na kampuni binafsi katika usambazaji
wa gesi asilia majumbani na kwenye magari (CNG), ambapo hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na
kuanza kutoa huduma.
Katika hatua nyingine, Homera amesema wiki ijayo Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za
utafutaji mafuta na gesi asilia (PSA)
kwa TPDC, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendelea na shughuli za utafutaji, uzalishaji na
uendelezaji wa rasilimali hizo nchini
ambapo Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi atakuwa mgeni rasmi.
Akizungumzia sekta ya umeme,
Mhe. Homera amesema uwezo wa uzalishaji wa
umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia,
jua na nishati nyingine mbadala,
huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka
2030.
Amesema katika kuimarisha
uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu,
Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II
wenye uwezo wa Megawati 100
ukiendelea.
Aidha, miradi mingine yenye uwezo wa zaidi ya
Megawati 600 ipo katika hatua
mbalimbali za majadiliano na upembuzi.
Kuhusu miundombinu ya
usafirishaji umeme, Waziri huyo amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao umeimarisha ubora na kiwango cha umeme
kinachofika katika mikoa yaMagharibi na Kaskazini mwa nchi.
Ameongeza kuwa Mradi wa
Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwaNovemba 2026 na kuunganisha Mkoa
wa Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara
ya kwanza, huku Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga ukitarajiwa kuwashwa Februari 2027 ili kuimarisha
upatikanaji wa umeme jijini Dar es
Salaam na maeneo ya viwanda ya Mkuranga.
Aidha, amesema utekelezaji wa
Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea
kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuondoa
changamoto za upatikanaji wa umeme
katika maeneo hayo.








0 comments:
Post a Comment