Meneja wa Fedha wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Ibrahim Mbinga, amesema usimamizi mbovu wa vipimo ndiyo adui mkubwa wa mfuko wa mfanyabiashara, mkulima na mnunuzi.
Akizungumza na wadau katika banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Nane Nane, Dodoma, Agosti 8, 2026 Meneja huyo amefafanua jinsi vipimo visivyo rasmi vinavyosababisha upotevu wa fedha usioonekana.
Mbinga ameeleza kuwa majukumu ya WMA yanalenga kuokoa wafanyabiashara, wakulima na walaji. “Watu wengi wanafikiri kupima kwa ndoo au visado ni rahisi. Lakini ukweli ni kwamba unajipiga risasi mguuni. Kila kilo, kila lita iliyopotea ni shilingi iliyotoka mfukoni mwako,” alisema.
Akidadavua kuhusu hesabu ya fedha kwenye vipimo, alisema vipimo ni sawa na mfuko wa fedha. “Gunia la mahindi kilo 100 ukiuza kwa ndoo 18 badala ya mizani, unapoteza kilo 10. Kama gunia ni shilingi 100,000, umepoteza shilingi 10,000. Ukiuza magunia 10 kwa wiki, umepoteza shilingi 100,000. Kwa mwezi ni milioni 1.2. Hiyo pesa ingekuwa wapi?” aliuliza.
Akieleza zaidi, alisema kuwa wafanyabiashara wengi hulalamika kupata hasara lakini akafafanua kuwa 'unaponunua mafuta lita 19 badala ya 20, au mpunga kilo 18 badala ya 20, unalipa pesa kamili na kupata bidhaa pungufu. Hiyo ni hasara ya moja kwa moja."
Akizungumzia mikopo kutoka Benki kwa wafanyabiashara wakulima alisema "Benki leo haziombi tu dhamana bali zinataka rekodi. Mkulima anayetumia mizani iliyohakikiwa na kuwa na risiti anaaminika zaidi. Vipimo sahihi vinakupa historia ya biashara yako ambayo benki inaitaka."
Aidha, Mbinga pia aliwaelimisha wafanyabiashara wakulima kuepuka gharama za faini ambazo husababisha hasara.
Akifafanua, alisema "kutumia vipimo visivyo rasmi ni kosa kisheria. Unapokamatwa unalipa faini na wakati mwingine bidhaa inaweza kuzuiliwa hivyo ni hasara mbili kwa wakati mmoja.
Badala yake, aliwashauri kuwekeza kiasi kidogo cha pesa kununua mizani iliyohakikiwa na WMA ili kujiepusha na faini inayoweza kukuletea hasara.
Katika hatua nyingine, Mbinga aliwashauri wafanyabiashara wakulima 'kujenga jina' ili kupata faida stahiki. "Mteja anapojua kuwa kwako anapata haki yake, atarudi tena na tena na ataleta wengine. Hiyo inakupunguzia gharama ya kutafuta wateja. Uaminifu unalipa," alisisitiza.
Meneja huyo wa Fedha, alihitimisha kwa kusisitiza kaulimbiu ya WMA isemayo "Pima kwa Haki, Pata Faida Halali" akidadavua kuwa mfanyabiashara akiwekeza kwenye mizani iliyohakikiwa leo, baada ya miezi miwili atashangaa tofauti yake kwenye akaunti yake ya fedha.
Mbinga amewataka wadau pia kutumia risiti na vitabu vya mauzo vinavyotokana na vipimo sahihi ili kufuatilia kwa urahisi mapato na matumizi.
Kwa upande wao, Wadau wameipongeza WMA kwa kuleta wataalamu wa fani mbalimbali katika banda la maonesho ya Nane Nane na kusema elimu ya kifedha imewapa uelewa mpya.










0 comments:
Post a Comment