Nafasi Ya Matangazo

August 08, 2026

Na Mwandishi Wetu
JAMII ya Wandondi na Wandwewe, imetoa mwito wa kitaifa na kimataifa kwa watu wote wenye nia njema kuungana katika Dua Maalum kwa ajili ya Amani, Umoja, Maridhiano, Mshikamano na Ulinzi wa Maisha ya Binadamu.

Dua hiyo ni mwito wa pamoja unaolenga kuwakutanisha watu wa imani, mila, tamaduni na mitazamo mbalimbali katika kusimama kwa pamoja Na Mwandishi Wetu amani, utu, uhai, mshikamano na heshima kwa mwanadamu, bila kujali tofauti za dini, kabila, rangi, taifa, utamaduni, itikadi au hali ya kijamii.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Chifu Felix G. L. Mfunda, kwa niaba ya jamii ya Wandondi na Wandwewe amesema dua hiyo itafanyika  Agosti 12, 2026,  ambapo Misa Maalumu ya Kikatoliki itafanyika katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Mhangazi, Parokia ya Kitanda, Namtumbo, Ruvuma. huku akitoa  mwito wa amani na maridhiano.

Aidha, kuanzia jioni ya Agosti 13 hadi mchana wa Agosti 14, 2026, kutafanyika dua, na shughuli za jadi zitakazoambatana na ngoma na sanaa mbalimbali za asili za Wandwele na Wandondi.

Jamii mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma, zikiwemo Makumbo, Lizombe na Makiwa, zinatarajiwa kushiriki katika shughuli hizo zinazolenga kuenzi urithi wa tamaduni, kuimarisha undugu na mshikamano, pamoja na kukuza amani kati ya jamii.

Mfululizo huo utakamilishwa Agosti 16, 2026, kwa Dua Maalumu ya Kiislamu itakayofanyika jioni kwa ajili ya kuiombea Tanzania, Afrika na dunia nzima.
Ambapo  amesema Dunia ya leo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo migogoro, vita, chuki, migawanyiko ya kijamii, changamoto za kiuchumi, ukosefu wa usawa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Katika mazingira haya, tunapaswa kutambua kwamba amani si wajibu wa Serikali pekee; ni wajibu wa kila mwanadamu.Tunatoa mwito kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wasomi, vijana, wanawake, mashirika ya kiraia na wananchi wote kutumia nafasi zao kujenga madaraja ya maelewano badala ya kuta za migawanyiko.

“Tunasisitiza umuhimu wa mazungumzo, kusikilizana, kusameheana, kuheshimiana na kutafuta suluhu za amani katika kila tofauti inayojitokeza.”

Aidha amesema ulinzi wa maisha ni wajibu wa pamoja akifafanua maisha ya mwanadamu ni tunu kubwa na hayapaswi kuwekwa rehani kwa sababu ya tofauti za kisiasa, kidini, kikabila, kiuchumi, kijamii au kiitikadi.

Ameongeza kwa msingi huo, wanatoa mwito wa kuheshimiwa kwa utu wa binadamu, haki ya kuishi, usalama wa raia na ulinzi wa watoto, wanawake, wazee na makundi yote yaliyo katika mazingira hatarishi.

“Tunasisitiza tofauti zetu zisigeuke kuwa sababu ya kupoteza maisha ya watu.Kila jamii ina wajibu wa kulinda maisha na kujenga mazingira ambayo kila mwanadamu anaweza kuishi kwa usalama.

Pia amesema kuhusu amani, afya na ulinzi wa mazingira ni kwamba amani ya kweli haiwezi kutenganishwa na afya ya jamii, usalama wa chakula, maji safi, mazingira salama na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

“Uharibifu wa mazingira, ukataji wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, upotevu wa bayoanuai na athari za mabadiliko ya tabianchi vinaweza kuongeza changamoto za kijamii na kiuchumi na kuhatarisha maisha ya watu.

“Kwa hiyo, tunatoa mwito wa kuunganisha juhudi za amani, afya, mazingira na maendeleo endelevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Akieleza zaidi amesema katika dua kwa Watanzania ,Afrika na Dunia amefafanua Tanzania iendelee kuwa taifa la amani, umoja, mshikamano na utulivu na kwa Afrika ipate amani na utulivu wa kudumu.

Pia migogoro na vita duniani zipungue na hatimaye kumalizika na kuongeza viongozi wapate hekima, busara, uadilifu na moyo wa kuhudumia watu.Vijana wapate fursa za elimu, ajira, ubunifu, ujasiriamali na maendeleo.

Kwa watoto walindwe dhidi ya ukatili, unyanyasaji na mazingira yanayohatarisha maisha yao. Wanawake, wazee na makundi yaliyo katika mazingira magumu walindwe na kuheshimiwa.Wagonjwa na wote wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali wapate faraja, matumaini na huduma stahiki na mazingira.

Kuhusu ujumbe kwa Watanzania amesema wanawakumbusha Umoja wetu ni nguvu yetu, amani yetu ni utajiri wetu, na maisha ya kila Mtanzania ni sehemu ya thamani ya Taifa letu.

“Tunapaswa kukataa chuki, uchochezi, ubaguzi, vurugu na lugha zinazogawa jamii. Badala yake, tujenge utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana, kusameheana, kusaidiana na kutatua tofauti zetu kwa njia za amani.

“Tanzania yenye amani na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya watu wake na mchango mkubwa kwa amani ya Afrika na dunia.”

 


Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo