MUFINDI: Wananchi wa vijiji vinavyopakana na Shamba la Miti Sao Hill wilayani Mufindi wameahidi kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuzuia na kudhibiti moto wa misitu, baada ya kupatiwa elimu kuhusu matumizi salama ya moto.
Ahadi hiyo imetolewa leo, Agosti 20, 2026, katika mikutano ya uhamasishaji iliyofanyika vijiji vya Bumilayinga na Kisada, Kata ya Bumilayinga, ikiwa sehemu ya kampeni za kila mwaka za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya moto na umuhimu wa kulinda misitu na mazingira.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Mwakilishi wa Mhifadhi Mkuu wa Tarafa ya Pili ya Shamba Ihefu, SCO Frank Milanzi, amesema wananchi wanaoishi karibu na shamba la miti wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha moto unaotokana na shughuli za kibinadamu hauingii katika misitu.
“Moto unaweza kusababisha madhara makubwa kwa misitu, mali na maisha. Ni muhimu kila mmoja kuhakikisha moto unaotumika kwa shughuli mbalimbali unadhibitiwa na kuzimwa kabisa baada ya matumizi,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Msitu Dhidi ya Moto wa Shamba la Miti Sao Hill, CO I Murya Sawa, amewataka wananchi kuacha kuwasha moto kiholela na kutoa taarifa mapema wanapoona dalili za moto katika maeneo ya misitu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bumilayinga, Mhe. Dorian Lyanzile, amesema viongozi wa vijiji na wananchi wanapaswa kuimarisha ushirikiano wao na TFS ili kuhakikisha matumizi ya moto hayahatarishi misitu na mazingira.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisada, Lidia Mwenda, amesema wananchi wamepokea elimu hiyo kwa umuhimu na wako tayari kushirikiana na TFS katika kulinda misitu, akieleza kuwa mikutano hiyo huwasaidia kutambua madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya moto.
Mikutano hiyo ni sehemu ya mpango wa TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka shamba hilo, ikiwemo vijiji 60 vinavyopakana nalo wilayani Mufindi, kwa kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kuzuia na kudhibiti moto, hasa wakati wa kiangazi.











0 comments:
Post a Comment