Huduma hizo zilitolewa Julai 28, 2026 katika Zahanati ya Serikali Kizwite, ambapo wananchi walipatiwa vipimo vya kisasa vya Ultrasound, uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, ushauri wa kitaalamu pamoja na dawa bila malipo. Huduma hizo ni miongoni mwa huduma ambazo kwa kawaida hazipatikani katika zahanati hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza dhana ya Polisi Jamii kwa vitendo kupitia ushiriki wake katika shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma zinazogusa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga, Dkt. Robert Lwebangila, aliipongeza Zahanati ya Polisi Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, akisema ushirikiano huo unaimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Afya Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edgar Ullaya, alisema lengo la zoezi hilo ni kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi na matibabu bila gharama pamoja na kugundua mapema changamoto za kiafya ili kutoa tiba stahiki.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Serikali Kizwite, Dkt. Simon Mjema, alisema huduma za Ultrasound zimeongeza uwezo wa zahanati hiyo kuwahudumia wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika vituo vingine vya afya.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Chanji, Dominica Mwaipopo, aliishukuru Serikali na Jeshi la Polisi kwa kuandaa huduma hiyo, akisema imepunguza gharama na muda ambao wananchi walikuwa wakitumia kutafuta matibabu.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma hizo walieleza kufurahishwa na hatua ya Jeshi la Polisi kusogeza huduma za afya karibu na makazi yao na kuomba zoezi hilo liendelee ili wananchi wengi zaidi wanufaike.
Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa za kuimarisha ushirikiano na jamii kupitia utoaji wa huduma za kijamii zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.









0 comments:
Post a Comment