Nafasi Ya Matangazo

June 25, 2026

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hania Bwahama akimuelezea Mshiriki wa mkutano mkuu wa tatu wa Kimataifa wa kikanda PEN-PLUS (ICPPA 2026) kutoka nchini Nigeria Mya Nyon vifaa vinavyotumika wakati wa upasuaji wa moyo alipotembelea banda la JKCI lililopo katika mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Msoka akimuelezea Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu kwa Umma Dkt Rahma Hingora kuhusu kampeni ya Jua Namba Zako inayofanywa na Taasisi hiyo alipotembelea banda la JKCI wakati wa mkutano mkuu wa tatu wa Kimataifa wa kikanda PEN-PLUS (ICPPA 2026) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hania Bwahama akimuelezea mtaalamu wa afya kutoka nchini Afrika Kusini Roylah Rykiel kuhusu huduma za upasuaji wa moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo wakati wa mkutano mkuu wa tatu wa Kimataifa wa kikanda PEN-PLUS (ICPPA 2026) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.
**************
Watalaamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameshiriki katika mkutano mkuu wa tatu wa Kimataifa wa kikanda PEN-PLUS (ICPPA 2026) ili kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kufikia maamuzi ya pamoja yatakayosaidia kufanikisha malengo ya afya kuelekea dira 2050.
Akizungumza wakati wa mkutano huo  Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Msoka alisema mkutano huo umesaidia kuwakutanisha wadau mbalimbali  kutoka nchi za Afrika  kujadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa hayo.
Dkt. Msoka alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi katika Bara la Afrika jambo linalohitaji hatua za haraka na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuyadhibiti.
“JKCI kama mdau katika mkutano huu tunashiriki kikamilifu katika kujadili changanmoto zilizopo na kutafuta suluhisho zake ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwani takwimu zinaonesha kuwa asilimia 35 ya vifo nchini vinatokana na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Msoka.
Dkt. Msoka alisema kupitia mkutano huo JKCI imeweka banda la maonesho kuwaonesha wataalamu kutoka nchi washiriki wa mkutano huo huduma inazozitoa na namna ambavyo imeleta mabadiliko makubwa katika matibabu ya moyo Afrika Mashariki na Kati.
“Kumekuwa na changamoto nyingi zinazotokana na mtindo usiofaa wa maisha katika ukanda wetu kama vile kutokufanya mazoezi, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutokufuata lishe bora, hizi ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia magonjwa yasiyoambukiza, hivyo sisi kama JKCI tunaendelea kupambana na magonjwa hayo katika jamii yetu”, alisema Msoka.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo waliotembelea banda la JKCI walipongeza jitihada za Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma za afya hususani huduma bingwa bobezi za magonjwa ya moyo.
“Huduma zinazotolewa na JKCI ni huduma za kiwango cha juu, naiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi wake hususani walioko vijijini ili wanapokumbana na changamoto za magonjwa ya moyo waweze kupata huduma kwa wakati”, alisema Padri Cosmas Mgina wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake Daktari kutoka nchini Ghana Wallace Ollen alisema JKCI imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
“Naipongeza JKCI kwani upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo Barani Afrika umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu kwa kuwa sasa hatuna sababu ya kusafiri kwenda mataifa mengine kama India kupata matibabu bingwa ya moyo”, alisema Dkt. Ollen.
Posted by MROKI On Thursday, June 25, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo