WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania, vyombo vya dola na taasisi nyingine zinazosimamia sheria, kudhibiti matumizi ya sarafu za kigeni katika uuzaji na ununuzi wa bidhaa na huduma nchini kwani ni kinyume cha Sheria.
“Sarafu rasmi kwa malipo halali ndani ya nchi yetu ni Shilingi ya Kitanzania, ni jambo la kisheria na ni jambo la kikatiba, kwa muongozo tulioutoa, malipo yote, kunukuu bei na matangazo yafanyike kwa shilingi ya Kitanzania”, amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 25, 2026) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Suma Fyandomo.
Fyandomo alitaka kujua mikakati ya Serikali katika kusimamia matumizi ya Shilingi ya Kitanzania katika huduma zote za kifedha nchini, ambapo Waziri Mkuu amesema matumizi holela ya sarafu isiyo ya Kitanzania ni kuvunja sheria.
“Wale wanaoweka bei za viwanja, ada, upangishaji wa nyumba, uuzaji wa huduma na maeneo mengine kwa dola au sarafu nyingine za kigeni wajue wanakiuka sheria yetu, na kwa kweli hawaitendei uzalendo nchi yetu ya Tanzania,” amesema Dkt. Mwigulu.
“Wengine wanafanya utakatishaji wa fedha chafu kwa kutangaza bei kwa sarafu za kigeni ili baadaye waonekane waliuza viwanja, lakini ni michezo michafu tu,” ameongeza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa kupitia muongozo uliotolewa na Serikali, hata taasisi za Serikali zimeacha matumizi ya sarafu za kigeni katika manunuzi na utoaji wa huduma na kuzitaka mamlaka kukomesha matumizi ya sarafu hizo za kigeni kinyume cha sheria.
“Nielekeze taasisi zetu zinazosimamia sheria, Benki Kuu ya Tanzania na Vyombo vya Dola, tuendelee kufuatilia mienendo ya aina hii, ili wale watakaotaka kunukuu bei ama kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni ili kuficha mambo mengine ikiwemo utakatishaji wa fedha haramu, tudhibiti vitu vya aina hiyo kwa sababu ni kinyume cha sheria,” amesema Dkt. Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Katika hatua nyingine Dkt. Mwigulu amezielekeza halmashauri ambazo ziko kando ya maeneo yanayoweza kutumika kwa ajili ya kuweka vizimba vya ufugaji wa samaki watumie fursa hiyo kuwawezesha wanawake kujihusisha na ufugaji huo kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.
“Tumieni ule utaratibu wa asilimia 4:4:2 ili kuweza kuwawezesha wanawake kushiriki katika uvuvi wa kutumia vizimba katika maeneo ambayo fursa hiyo ipo”
Waziri Mkuu ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Mwakyembe aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wanawake kupata vizimba vya kuzalishia samaki katika maeneo yote ya bahari, mito na maziwa ambapo Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi, na wanawake wakiwa ni miongoni mwa wanufaika.
“Takriban miaka miwili au mitatu iliyopita, Mheshimiwa Rais alizindua zoezi la kugawa vizimba kwa vijana wa Tanzania. Zoezi hilo linahusisha vijana wote wa kike na wa kiume, kwa hiyo zoezi hilo lilihusisha pia wanawake,” ameeleza Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa, kwa upande wa bahari na maeneo mengine zoezi hilo linaendelea, likiwa linafanyika kwa majaribio, na uwekezaji mkubwa wa bandari ya uvuvi iliyopo wilayani Kilwa, utachochea zaidi mpango huo kwa kuwa kutakuwa na mahitaji makubwa ya malighafi.
“Mheshimiwa Mbunge nakuhakikishia, Serikali inaweka mkazo katika jambo hilo, na kule tunakokwenda utakuwa ni uvuvi wa kawaida katika maeneo mengi ili kuweza kuwawezesha vijana na wanawake wengi pamoja na makundi maalum kujihusisha na shughuli hizo,” amesisitiza Waziri Mkuu.






0 comments:
Post a Comment