WIZARA ya Madini imevuka lengo la ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 baada ya kukusanya Sh trilioni 1.27 hadi Juni 5, 2026, dhidi ya lengo la Sh trilioni 1.2, huku ikitarajia kufikia Sh trilioni 1.3 ifikapo Juni 30, 2026.
Kutokana na mafanikio hayo, watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake wametakiwa kuondokana na uzembe, kuongeza bidii na kufanya kazi kwa weledi ili kufikia lengo jipya la ukusanyaji wa Sh trilioni 1.4 lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza katika kikao cha watumishi wote wa Wizara ya Madini na taasisi zake ambazo ni GST, TEITI, Tume ya Madini, STAMICO na TGC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, amesema mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi katika usimamizi wa Sekta ya Madini kwa kuzingatia Sera, miongozo, kanuni na Sheria zilizowekwa.
Amesema watumishi wanapaswa kutambua kuwa wanapowahudumia wananchi wanatekeleza wajibu wenye thamani kubwa kwa taifa, hivyo wanapaswa kuwahudumia watu wote kwa usawa bila kujali itikadi, dini wala uraia wao.
“Wachache tuliokabidhiwa jukumu la kuhudumia sekta ya madini tunapaswa kuhakikisha watu wote wanahudumiwa kwa haki na uzalendo mkubwa ili kuendelea kujenga taifa letu,” amesema.
Amesema watumishi ndiyo injini ya Serikali katika sekta ya madini na kwamba mchango wao una nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia usimamizi bora wa rasilimali madini.
“Wito wangu ni kufanya kazi kwa bidii, weledi na kusimamia sera, miongozo, kanuni na sheria zilizowekwa ili sekta hii iendelee kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa,” amesema.
Katibu Mkuu huyo amesema watumishi wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa, uvivu na uzembe ambavyo vinaweza kuharibu imani ya wananchi kwa wizara, taasisi zake na Serikali kwa ujumla.
“Tusiharibu imani ya wananchi kwa rushwa, uvivu na uzembe. Mtu mmoja anayepokea rushwa anaweza kuchafua kazi za watumishi wengi waadilifu. Tufanye kazi kwa uzalendo mkubwa ili kuhakikisha hakuna mtu au wachache miongoni mwetu wanaochafua taswira ya wizara, taasisi zetu na Serikali kwa ujumla,” amesema.
Amesema watumishi wanapaswa kuchagua kuwa mwangaza badala ya kuwa kivuli na kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya wizara na taasisi zake kwa kuwa wote ni timu moja yenye malengo yanayofanana.
“Kazi ya mwenzako ikichelewa, mafanikio yako pia yanachelewa. GST ikichelewa kutekeleza majukumu yake, Tume ya Madini nayo itaathirika. Tusaidiane kwa pamoja kufikia malengo yetu,” amesema.
Katika salamu za Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, watumishi wamepongezwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha, imeelezwa kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imepangiwa kukusanya Sh trilioni 1.4, lengo ambalo linahitaji watumishi kuongeza uwajibikaji, uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.











0 comments:
Post a Comment