Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi, amesema Maonesho ya Kimataifa ya Karibu-KiliFair 2026 yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.
Maonesho hayo mbali na kutangaza utalii pia, yanatoa nafasi ya kuonesha vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo utalii wa misitu, kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuvutia uwekezaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo uliofanyika Juni 5, 2026 katika Viwanja vya Magereza mkoani Arusha, Dkt. Mugobi alisema Karibu-KiliFair imekuwa nyenzo muhimu ya kutangaza utajiri wa rasilimali za utalii zinazopatikana nchini na kufungua masoko mapya ya sekta hiyo.
Alisema maonesho hayo yanatoa fursa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha bidhaa na huduma zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kuimarisha ushirikiano unaochochea ukuaji wa sekta ya utalii.
“Karibu-KiliFair si maonesho ya kawaida bali ni uwekezaji wa kimkakati unaosaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, kuvutia wawekezaji wapya na kufungua masoko mapya ya bidhaa na huduma za utalii,” alisema Dkt. Mugobi.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yanaendelea kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi, jambo linalochangia kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Dkt. Mugobi alisema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na huduma za malazi ili kuongeza urahisi wa kufikia maeneo ya vivutio na kuboresha uzoefu wa watalii.
Pia alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuitangaza Tanzania kwenye masoko ya kimataifa, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza mwonekano wa vivutio vya nchi na kuwafikia watalii wengi zaidi duniani.
Katika maonesho hayo, taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), zinashiriki kutangaza huduma na fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo ya utalii wa mazingira na misitu ya hifadhi.
Karibu-KiliFair 2026 inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama moja ya maonesho makubwa ya biashara ya utalii Afrika Mashariki, ikitoa jukwaa la kukuza ushirikiano, uwekezaji na utangazaji wa vivutio vinavyoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa utalii barani Afrika.










0 comments:
Post a Comment